Habari

Imewekwa:: Jun, 10 2021
News Images

KAMPUNI THELATHINI (30) ZAJITOKEZA KUNUNUA PAMBA MSIMU WA 2021-22

Msimu wa ununuzi wa pamba mbegu umezinduliwa mnamo tarehe 10 Mei 2021 ukiashiria kuanza rasmi kwa ununuzi wa pamba kwa kanda ya uzalishaji pamba Magharibi inayojumuisha mikoa kumi na moja (11) mingi kati ya mikoa hiyo ikiwa ni ya Kanda ya ziwa ambayo inakadiriwa kuzalisha takribani 99% ya pamba yote nchini.

Katika msimu huu wa ununuzi/uzalishaji wakulima wanatarajia kuvuna kiasi cha tani 390,000 za pamba mbegu na maeneo karibu yote ya uzalishaji kanda ya magharibi wakulima wanaendelea na uvunaji na uuzaji pamba vilevile uchakataji wa pamba iliyonunuliwa ukiendelea katika viwanda vya kuchambua pamba

Soko la pamba mbegu nchini ni la uhakika kutokana na mifumo mizuri na endelevu iliyowekwa na serikali ambapo haijawahi kutokea hata msimu mmoja wakulima wakakosa soko la kuuza pamba yao baada ya kuvuna. Uimara huu wa mfumo wa soko la pamba umepelekea wakulima wengi kuendelea kulima pamba kwa ushindani wa ubora na jitihada za kuongeza tija Zaidi ili kuweza kujiongezea kipato na kushawishi wanunuzi waendelee kuichagua pamba ya Tanzania.

Wakati ununuzi ukiwa umefikia wiki ya nne (4) na uchambuaji pamba ukiendelea tasnia ya pamba imeendelea kuhakikishia wakulima soko la pamba ambapo katika msimu huu wa soko jumla ya makampuni thelathini (30) ya uchambuaji pamba yamejitokeza kununua pamba yote itakayozalishwa na wakulima nchini. Kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na serikali kila mnunuzi atakayeingia sokoni anatakiwa atoe bei ya ushindani kwa kuanzia bei dira iliyotangazwa Tsh 1050 kwa kilo moja ya pamba mbegu daraja A (pamba safi) na Tsh 525 kwa kilo moja ya pamba mbegu daraja B (pamba fifi).

Akizungumza kwa nyakati tofauti Katibu Mkuu wa Chama cha wanunuzi wa pamba nchini (TCA) Bw. Boaz Ogola ameelezea kuwa bado kuna kiu kubwa kwa wanunuzi haijatimizwa kwa kuwa kiasi cha pamba kinachozalishwa kutotosheleza mahitaji yao wanunuzi hali inayochangiwa na tija kuwa chini. Katibu Mkuu huyo wa TCA amesema wanunuzi kwa umoja wao na uwezo wa viwanda vyao wana mahitaji ya tani milioni moja (1,000,000) wakati uzalishaji wa pamba mbegu msimu 2021-22 ukikadiriwa kati ya tani laki tatu hadi tani laki nne tu hivyo kupelekea viwanda vingi kufanya kazi chini ya uwezo wao. Ili kuweza kuifanya pamba iendelee kutupamba (kuboresha maisha ya wakulima na kukuza uchumi) Bw. Ogola amesisitiza wakulima pamoja na wadau wote wa sekta ndogo ya pamba kwa ujumla kujikita katika kuongeza tija