Habari

Imewekwa:: Mar, 09 2023
News Images

BODI YA WAKURUGENZI TCB WATEMBELEA WAKULIMA WA PAMBA

Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Bodi ya Pamba Tanzania chini ya Makamu Mwenyekiti wake Aggrey Mwanri ambaye pia ni Balozi wa zao ilo nchini wametembelea mashamba ya pamba na kukutana na wakulimakatika wilaya za Bariadi, Busega, Itilima, Meatu na Maswa mkoa wa Simiyu ambapo katika ziara hiyo wameoneshwa kuridhishwa na hali ya maendeleo ya zao la pamba shambani na juhudi za wakulima katika utunzaji mashamba.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Makamu Mwenyekiti Ndg. Mwanri aliwaasa wakulima pamoja na uongozi wa mkoa wa Simiyu kuzingatia vema kanuni za kilimo bora cha pamba pamoja na sheria ya pamba ya mwaka 2001 inayosisitiza ungoaji wa masalia ya pamba kabla ya kupanda pamba na kuzuia uchanganyaji pamba na mazao mengine katika mashamba

Mwanri ameridhishwa na jitihada zinazofanywa na TCB katika kusimamia na kuleta maendeleo endelevu kwa tasnia ya pamba nchini huku akishauri wakulima wa pamba wote nchini kuendelea kuhudumia zao hasa upuliziaji viuadudu kwa kipindi chote cha msimu kwa kuwa serikali inaendelea kuweka nguvu nyingi katika usambazaji pembejeo muhimu na utoaji elimu kwa njia mbalimbali

Wajumbe wa Bodi iyo walipata fursa ya kuzungumza na wakulima waliokuwa mashambani na kupokea na kuwapa ushauri na changamoto mbalimbali ambazao zikitatuliwa zitafanya sekta iwe na maendeleo endelevu. Miongoni mwa changamoto zilizotolewa na wakulima ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi hali inayopelekea ukame ambao unaathiri uzalishaji na kipato chao kwa ujumla.

Akizungumzia changamoto ya uhaba wa mvua mkulima Bw. Juma Kabelege maarufu JB wa kijiji cha Dutwa wilaya ya Bariadi alisema mvua zimekuwa hazitabiriki vizuri hali inyopunguza mavuno na kipato kwa kuzingatia uwekezaji mkubwa wanaofanya katika kulima na kutunza mashamba yao

Akitoa ushauri wa namna ya kukabiliana na changamoto ya ukame mjumbe wa Bodi Dkt. Riyaz Haider ameshauri wakulima kuanza kufikiria kuanzisha miundo mbinu rahisi ya umwagiliaji kwa kutumia mabwawa ya kuvuna na kutunza maji ya mvua ambayo hupotea wakati upo uwezekeno wa kunufaika nayo kwa kumwagilia mazao

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa Bodi ya Pamba Tanzania akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Ndg. James Shimbe alitoa rai kwa wakulima viongozi au wakulima wawezeshaji kuwatembelea wakulima wengine wanaowafundisha ili kuona utekelezaji wa elimu wanayowapatia

“Wataalam wetu hawatoshi na sio wengi kiasi kile kuweza kuwepo kila kijiji na ndio maana tunawafundisha wakulima wawezeshaji wawili (2) katika kila kijiji waweze kutoa msaada”

Shimbe alisema Bodi ya Pamba imewezesha wakulima wawezesha 2,500 baiskeli kama nyenzo ya usafiri kuwafikia wakulima wengine kwa ngazi ya kijiji

Mkaguzi wa pamba wa wilaya ya Bariadi Ndg. Thadeo Mihayo naye alikiri kuwa wakulima wawezeshaji wamekuwa na msaada mkubwa sana katika utendaji kwa kufanya mawasiliano kwa wakati na wataalam kwa ajili ya utatuzi wa haraka wa changamoto mbalimbali katika uzalishaji pamba

Lengo kuu la ziara ya Wakurugenzi wa Bodi ni kufuatilia utekelezaji wa lengo la kufikia uzalishaji tani 1,000,000 (milioni moja) za pamba ifikapo 2025/26 na kujionea maendeleo ya msimu wa pamba 2022/23 wakati bodi hiyo ikitarajiwa kufanya kikao chake maalum cha 44 mjini Bariadi mkoa wa Simiyu ambao ni mkoa kinara katika uzalishaji wa pamba nchini.