Habari

Imewekwa:: Jul, 03 2022
News Images

WAKULIMA TULIME PAMBA KWA VIWANGO 30/60

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu amesema hayo tarehe 2 Julai,2022 wilayani Tanganyika Mkoani Katavi wakati akifunga hafla fupi ya Siku ya Shambani “Field Day “ iliyowakutanisha wakulima pamoja na wataalam wa kilimo kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Katavi iliyoandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) kwa ushirikiano na mradi wa “Cotton Victoria” chini ya ufadhili wa serikali ya Brazili


Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Mhe. Onesmo Buswelu akizungumza na wakulima wa pamba siku ya Shamba darasa "Feld day"

Wakulima na wataalam wa Kilimo kutoka mkoa wa Katavi wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika siku ya Shamba darasa iliyoandaliwa na mradi wa Cotton Victoria

Bw.Ramadhani Nyembe mkulima wa pamba wa kijiji cha Majalila wilayani Katavi akitoa ufafanuzi namna alivyohudumia shamba lake kwa kutumia teknolojia bora na vipimo vipya vya upandaji mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika,wakulima na wataalam wa Kilimo

Shamba la mkulima wa pamba Bw. Ramadhani Nyembe lililopo kijiji cha Majalila Tanganyika lililopandwa kwa vipimo vipya vya sentimeta 30 kwa sentimeta 60 likiwa limekomaa vizuri tayari kwa kuvunwa

Mhe. Buswelu ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo aliwaasa wakulima kutumia teknlojia mpya ya nafasi za upandaji kilimo cha pamba inayofundishwa na wataalam kwa vitendo ili kuweza kujiinua toka katika tija duni ya kilimo cha pamba ambapo upata kilo 300-700 kwa ekari hadi kufikia kuzalisha kilo 1400-2000 kwa ekari

“Kwa muda mrefu wakulima wamekuwa na shauku ya kuyaona matokeo ya utafiti,leo tunapata fursa ya kuona matokeo hayo shambani hapa shukrani sana kwa kituo cha TARI”

“Taasisi ya TARI inafanya tafiti hizi kwa lengo la kukufanya mkulima uzalishe pamba yako kwa tija itakayopelekea kukuongezea kipato lakini vilevile kama nchi tutanufaika kwa kuwa na malighafi za kutosha katika viwanda vyetu,mzunguko huo wa malighafi utatuwezehsa kutengeneza fursa za ajira kupitia viwanda”


“Wakulima wa pamba wa mkoa wa Katavi na maeneo mengine nawaasa msipande pamba chini ya viwango,yaani nafasi inayopendekezwa ya sentimeta 60 kwa sentimeta 30.Ukipanda chini ya kiwango utakuwa unajiibia mwenyewe kwa kuwa utapata mavuno chiniya yale wanayopata wanaozingatia viwango. Kama mkulima ukikosa pamba bai iwe tu kwa sababu nyingine ambazo ziko nje ya uwezo wa wataalam ila sio sababu haukufuata viwango”

Mhe Buswelu amewapa rai wakulima kuhakikisha wanawatumia ipasavyo wataalam wa kilimo kwa kuwa serikali inawaandaa kwa gharama hadi kufikia hapo hivyo ni budi kuwatumia ipasavyo ili kujikwamua kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa kinachozingatia matumizi ya teknolojia

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine mkulima wa Kijiji cha Majalila wilayani Katavi Bw. Ramdhani Nyembe ambaye hafla hiyo ilifanyika katika shamba lake ametoa ushuhuda wake kuwa kwa kutumia vipimo vya sentimeta 30 kwa 60 katika msimu huu amefanikiwa kupata mavuno mengi kulinganisha na misimu iliyotangulia. Vivile Bw. Nyembe amewahasa wakulima wenzake kufuata teknolojia hii mpya ya upandaji kuweza kujiongezea mapato kwani hali wameiona katika shamba lake ambapo anatarajia kupata Zaidi ya kilo 1200 kwa ekari

Kwa upande wake mratibu wa zao la pamba nchini Dkt Paul Saidia ambaye pia ndio msimamizi wa mradi wa Cotton Victoria Tanzania ameelezea mafanikio ambayo yamefikiwa tangu mradi huu utambulishwe hapa nchini mwaka 2017. Ambapo hadi sasa jumla ya mikoa saba(7) ya Mwanza,Simiyu,Geita,Tabora,Katavi,Mara na Shinyanga imeshafikiwa na maafisa ugani sita kutoka kila wilaya walipata mafunzo hivyo amewahasa waendelee kupeleka ujumbe zaidi kwa wakulima ili kuweza kuleta mageuzi katika kilimo cha pamba hapa nchini

Naye Bw. Renatus Luneja Afisa Kilimo Mwandamizi kutoka Bodi ya Pamba akimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania aliwatoa hofu wakulima kwa kuwahahakishia kuwa Bodi inaenda sambamba na mabadiliko haya ya teknolojia kwa kuhakikisha kuwa mahitaji ya pembejeo yanatosheleza na kumfikia mkulima kwa wakati.