Habari

MSIMU WA UNUNUZI 2025/2026 WAZINDULIWA UZINGATIAJI WA UBORA WA PAMBA UKIPEWA KIPAUMBELE
Msimu wa ununuzi wa pamba nchini kwa mwaka 2025/2026 umezinduliwa rasmi tarehe 2 Mei 2025 katika Mtaa wa Mwakibuga, Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu. Sherehe hii ya uzinduzi ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Kenani Laban Kihongosi, ambaye alikuwa mgeni rasmi na aliyetangaza kuanza rasmi kwa msimu huu muhimu wa kilimo cha pamba.
Katika hotuba yake, Mhe. Kihongosi alitangaza bei elekezi ya pamba kwa msimu huu kuwa Shilingi 1,150 kwa kilo moja kwa pamba daraja A na shilingi 575/= kwa pamba daraja B. Mkuu huyo wa mkoa amesema bei hizi zimewekwa ili kuhakikisha wakulima wanapata faida inayolingana na jitihada zao, huku serikali ikisisitiza ushindani wa haki katika soko la pamba kama sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Kihongosi aliwataka watendaji wa vyama vya ushirika (AMCOS) kuwa waaminifu katika ununuzi wa pamba, akielezea kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wanaonyonya wakulima kwa kuwapa bei zisizo halisi, hasa wakati bei za pamba zinapopanda kutokana na mazingira ya ushindani. Alisema, “Wapo wengine bei ikipanda hawawalipi wakulima. Serikali itachukua hatua kali dhidi yao.”
Aidha, alitoa rai kwa wanasiasa kutoingilia mchakato wa usambazaji wa pembejeo za kilimo, akisisitiza kuwa jukumu hilo liachwe kwa watendaji na wataalam walioteuliwa na serikali. Hii ni kudhibiti wizi na upotevu wa pembejeo, kama ilivyojitokeza katika msimu wa kilimo wa 2024/2025, ambapo Wilaya ya Bariadi pekee ilikamata mbegu za pamba za wizi zilizotakiwa kwenda kwa wakulima kiasi cha tani 148,150 zenye thamani ya Shilingi milioni 207. Kesi ya wizi huo bado inaendelea mahakamani.
Wakati wa sherehe hizo za uzinduzi wa Msimu wa pamba serikali imetangaza kuaza rasmi kwa matumizi ya mizani janja msimu wa ununuzi 2025/2026 ikiwa na lengo la kuweka uwazi, kupunguza wizi, na kuhakikisha wakulima wanapata haki yao. Mizani hii itasaidia kupunguza mianya ya udanganyifu inayofanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu ambao wamekuwa wakipunja wakulima kwa kuchezea mizani.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Ndg. Marco Mtunga, alisema kuwa ubora wa pamba ni muhimu sana ili wakulima wapate bei bora sokoni. Alielezea kuwa uchafu au utunzaji dhaifu wa pamba unaathiri sifa yake katika soko la kimataifa, hali inayoweza kupunguza bei. Alisema, “Wakulima wa pamba hawawezi kupata bei nzuri kama hawazingatii ubora wa pamba.”
Kwa msimu ujao wa kilimo, Mtunga aliahidi kuwa maafisa wa kilimo watasaidia wakulima kutengeneza mbolea ya kupulizia ya maji, ambayo itawasaidia kuongeza tija kwa gharama nafuu. Mbolea hii itasaidia kuboresha uzalishaji wa pamba huku ikihakikisha wakulima wanapata mavuno bora zaidi.
"Bodi ya Pamba tunasisitiza mkulima alime kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu, ili kuongeza tija. Tatizo siyo bei ndogo ya pamba, bali ni uzalishaji usio na tija. TCB tunaendelea kutoa elimu ya kilimo chenye tija,"
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, ambaye ndio mwenyeji wa sherehe hizo ameyasihi makampuni ya ununuzi wa zao la pamba kununua zao hilo kwa ushindani, ili kupata malighafi hiyo na wakulima wanufaike. "Ninawaomba na kuonya kwa mkulima yeyote wa pamba, asijaribu kuweka maji wala mchanga wakati anapotaka kuuza pamba yake. Atakayebainika lazika ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria za nchi,"
"Ninawaomba na kuonya kwa mkulima yeyote wa pamba, asijaribu kuweka maji wala mchanga wakati anapotaka kuuza pamba yake. Atakayebainika lazika ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria za nchi,"