WAKULIMA WAPONGEZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KILIMO CHA PAMBA
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania ilinunua jumla ya mitambo 16 ya kisasa (self-propelled boom sprayers) kwa ajili ya kurahisisha shughuli za upuliziaji na udhibiti wa wadudu waharibifu wa zao la pamba.
Mitambo hiyo imekwishasambazwa katika wilaya tano (5) kati ya wilaya nane (8) za kimkakati katika uzalishaji wa pamba ambazo ni:Meatu, Maswa, Kishapu, Igunga na Bariadi
Lengo kuu ni kuhudumia wakulima wenye mashamba makubwa ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuokoa muda wa uzalishaji. Akizungumza kuhusu mpango huo, Bw. Ndinda Anthony Afisa Kilimo wa Bodi wilaya ya Bariadi, alisema:“Serikali imenunua na kusambaza mashine hizi kwenye wilaya za kimkakati kwa uzalishaji wa pamba, zikilenga kuhudumia wakulima wenye mashamba makubwa. Mashine hizi zinawahudumia wakulima waliopanda kwa kuzingatia kanuni za kilimo cha pamba ikiwemo kupanda kwa mistari, kwani mtambo huu huendesha na kupitia shambani ukipulizia dawa kwa ufanisi.”
Alisisitiza kuwa matumizi ya mitambo hiyo yanahitaji wakulima kufuata kanuni bora za kilimo ili kuongeza tija na kuhakikisha dawa inatumika kwa usahihi.
Awali wakizungumza na waandishi wa habari waliofanya ziara katika Kijiji cha Kasoli, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, wakulima waliipongeza Serikali kwa kuleta teknolojia za kisasa zinazorahisisha shughuli za kilimo. Marco Kayanhale, mkulima na mkazi wa Kijiji cha Mwamlapa, alisema: “Miaka ya nyuma tulikuwa tunapulizia kwa solo la mgongoni. Katika shamba hili nilikuwa natumia siku nne kupulizia na kuchoka sana. Sasa Serikali imetuletea mashine ya kupulizia — tumeona imerahisisha kazi sana. Nitapunguza gharama za vibarua na muda wa kukaa shambani.”
Aliongeza kuwa ujio wa mitambo hiyo utasaidia kuongeza tija na kupunguza uchovu uliokuwa unatokana na matumizi ya pampu za mgongoni.
Naye Marco Kubagwa, mkulima wa Kijiji cha Nyanguge, wilayani Bariadi, alisema: “Mashine hizi zinarahisisha sana upuliziaji kwa wakulima wenye mashamba makubwa. Zamani tulitumia pampu za mgongoni ambazo zilileta uchovu na maumivu, lakini sasa mashamba makubwa yanapuliziwa kwa muda mfupi.”
Afisa Kilimo kupitia Mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika Kijiji cha Mwamlapa, Chongela Selemani, alisema; “Mashine hizi zimerahisisha kazi kwa kiasi kikubwa. Awali wakulima walikuwa wanatumia siku mbili hadi tatu kumaliza kupulizia shamba la ekari moja.”
Aliongeza kuwa licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya baadhi ya wakulima kutokuzingatia kanuni za kilimo bora hususan kupanda kwa mistari. Hata hivyo, maafisa ugani wanaendelea kutoa elimu kupitia mashamba darasa ili wakulima wapande kitaalamu na waweze kunufaika kikamilifu na teknolojia hiyo.
Ununuzi na usambazaji wa mitambo hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uzalishaji wa pamba, kuongeza tija kwa mkulima na kuendeleza kilimo cha kisasa kinachotumia teknolojia.