IGUNGA YAANZA MAANDALIZI UZALISHAJI MBEGU BORA KWA WAKULIMA

Maandalizi ya msimu mpya wa kilimo cha pamba 2025/2026 yameanza maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa pamba nchini. Wilaya ya Igunga mkoani Tabora ambayo ni wilaya kitalu cha uzalishaji wa mbegu bora za pamba wakulima wanaendelea kusafisha mashamba kwa kung’oa masalia ikiwa ni mojawapo kati ya kanuni kumi (10) za kilimo bora cha pamba.
Serikali ya wilaya ya Igunga ikishirikiana kwa karibu na Bodi ya Pamba inasimamia mikakati ya kuhakikisha inazalisha zao la pamba kwa tija ili kuendelea kuwapa uhakika wa mbegu bora wakulima wanaolima pamba maeneo yote nchini misimu ijayo. Mikakati hiyo ni pamoja na kusimamia wakulima kuhakikisha wanazingatia kanuni ya kumi (10) ya kilimo bora cha pamba inayotaka wakulima wote kung’oa na kuchoma moto masalia ya pamba kabla au ifikapo tarehe 30 Septemba 2025.
Akizungumza ofisini kwake hivi karibuni Mkuu wa wilaya ya Igunga Mhe. Sauda Mtondoo akitoa ujumbe mahususi kwa wakulima amesema “Wakulima wote kuhakikisha wanangoa na kuchoma masalia yote ya pamba ikiwa ni sehemu mojawapo ya kutekeleza kanuni za kilimo bora cha pamba. Kutofanya hivyo madhara yanakuwa makubwa, wadudu wanakuwa wengi na kusababisha pamba inayozalishwa inakuwa sio bora na ukizingatia sisi ni kitalu cha mbegu na wakati wote tunapaswa kuwa makini kuhakikisha tunazalisha mbegu bora kwa ajili ya wakulima wa maeneo mangine. Mkuu huyo wa wilaya ametoa rai kwa wale wote ambao hawajatekeleza ilo waanze mara moja kusafisha mashamba yao kujiandaa na msimu wa kilimo kabla serikali haijaanza kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria ya pamba Na. 2 ya mwaka 2001.
Nao wakulima wa pamba Bw. Lucas Sitta na Bi. Flora Masunga kutoka kata ya Mbutu wilaya ya Igunga wamezungumzia jinsi walivyojiandaa kuelekea msimu mpya wa Kilimo 2025-2026. “Tumeshaanza kuandaa mashamba tunayatayarisha tuko vizuri na mwitikio wa sasa ni mzuri kuliko ule wa zamani watu walikuwa wagumu lakini sasa hivi elimu inaenda vizuri watu wameshakuwa waelewa pia hata bila kuwahamasisha sana masalia wameanza kukata wenyewe mashamba yapo vizuri na matangazo ya kuandaa mashamba tunayasikia na tunazidi kuhamasika Zaidi
Afisa Kilimo wa kata ya Mbutu kupitia Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) Bi. Nice Thomas amesema “Zoezi la kusafisha mashamba linaenda vizuri huku tukihakikisha tunawatembelea wakulima mmoja tunawamasisha, tunafanya nao mikutano tunawaelekeza, magari ya matangazo yanapita kila mara kuhamasisha ukataji masalia na mwitikio wao ni mzuri”