Habari

Imewekwa:: Apr, 22 2025
News Images


Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora ambao sehemu kubwa iliundwa na wajumbe wa kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira ya ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Sauda Mtondoo, imefanya ziara katika baadhi ya viwanda vya kuchambua pamba vilivyoko mkoani Shinyanga,ili kubaini changamoto za usafi na ubora wa pamba.

Ziara hiyo ni sehemu ya ufuatiliaji juu ya malalamiko ya kushuka kwa ubora wa pamba iliyozalishwa wilayani humo katika msimu wa kilimo uliopita wa mwaka 2023/2024 kutoka kwa wamiliki wa viwanda vya kuchambua pamba na takwimu za Bodi ya Pamba ambapo zinaonesha ubora umeshuka kwa takribani 21%.

Katika ziara hiyo, kamati ilitembelea viwanda vya Fresho Investment LTD, GAKI Investment Ltd na Afrisian Ginning Ltd na baadhi ya wamiliki na wasimamizi wa viwanda wakiwemo Benny Nkya, Msimamizi wa Kiwanda cha Fresho Investment, na Gasper Kileo, mmiliki wa Kiwanda cha Gaki Investment, walieleza kuwa msimu uliopita uligubikwa na changamoto kubwa ya upokeaji wa pamba chafu.

Wamesema pamba hiyo ilikuwa imechanganywa na mchanga, maji, vikonyo vya pamba na mara nyingine kulikuwa na udanganyifu wa uzito, hali ambayo inadaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika na masoko(AMCOS) wakati wa ununuzi.

Baada ya kubaini hali hiyo, wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Lucas Moga, wametoa msimamo wa pamoja kuhakikisha hali ya uchafuzi wa pamba inadhibitiwa.

Wamesisitiza umuhimu wa utoaji wa elimu kwa wakulima pamoja na viongozi wa AMCOS kuhusu uzalishaji na usimamizi bora wa zao la pamba, ili kuhakikisha pamba inayofika viwandani inakuwa safi na yenye ubora.

Kaimu Meneja wa Bodi ya Pamba Kanda ya Magharibi, Mhandisi Kisinza Ndimu, amethibitisha ongezeko la uchafuzi wa pamba katika msimu uliopita wa 2023/2024, na kueleza kuwa Bodi hiyo imeamua kushirikiana na serikali katika kushughulikia tatizo hilo kwa pamoja, hasa ikizingatiwa kuwa linaanza kuathiri masoko ya nje ya nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Igunga Mapunda Temanya, ameeleza kuwa chanzo kikuu cha tatizo hilo hakipo kwa wakulima moja kwa moja, bali ni kwa baadhi ya viongozi wa AMCOS wasio waaminifu.

Akizungumza wakati akihitimisha ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo, amewataka madiwani na viongozi wote wa serikali kuhakikisha wanawajibika ipasavyo katika maeneo yao,kuhakikisha pamba inayozalishwa na kuingia kwenye mfumo wa ununuzi ni safi na yenye ubora.

Ametoa onyo kali kwa mtu yeyote atakayebainika kuchafua au kuharibu pamba, akisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa kuwa hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya mnyororo wa thamani wa zao hilo nchini.

Ametoa onyo kali kwa mtu yeyote atakayebainika kuchafua au kuharibu pamba, akisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa kuwa hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya mnyororo wa thamani wa zao hilo nchini.