Habari

Imewekwa:: May, 05 2023
News Images

Msimu wa ununuzi wa pamba 2023/2024 nchini umezinduliwa rasmi wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma ukiashiria kuanza rasmi kwa uuuzaji na unuuzi wa pamba ya wakulima nchini

Uzinduzi huu unatoa nafasi kwa wakulima, wanunuzi, ushirika pamoja na viongozi wa serikali kukutana na kupata ufahamu wa pamoja juu ya masuala muhimu ya ununuzi wa pamba kabla msimu wa ununuzi haujaanza

PICHANI : Wakulima wa kijiji cha Rungwe Mpya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wakifuatilia sherehe za uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba 2023/24

Akihutubia katika halfa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi aliipongeza Bodi ya Pamba Tanzania kwa kutambulisha teknolojia mpya ya upuliziaji viuadudu kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

Kanali Mwakisu alisema kuwa “wakulima wa pamba hasa wenye mashamba makubwa wamekuwa na changamoto ya kudhibiti wadudu waharibifu kwa ufanisi kutokana na matumizi ya mabomba ya mgongoni kutokuendana na maeneo wanayo yahudumia hivyo ujio wa teknolojia hii utatatua tatizo hilo na kuwavutia wakulima wengi zaidi kuongeza maeneo ya uzalishaji”

PICHANI: Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu akikabidhi fedha kwa mkulima wa kwanza kuuza pamba msimu wa ununuzi 2023/24

Katika uzinduzi huo mgeni rasmi alitangaza bei elekezi ya pamba mbegu kwa msimu wa 2023/24 kuwa ni Shilingi 1060/=.ikiwa ni bei ya kuanzia na wakulima hawapaswi kuuza pamba chini ya bei hiyo. Bei ya msimu huu imepungua kutoka bei elekezi ya shilingi 1560/= ambayo wakulima waliipata katika msimu wa 2022/23

Baadhi ya wakulima wakipokea bei hiyo hawakuacha kutoa maoni yao kuwa bei si rafiki kwao kulinganisha na gharama za uzalishaji kuwa kubwa hivyo kuomba serikali ione namna ya kutatua changamoto hii kwa kuongeza bei

Akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa msimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Ndg. Marco Mtunga amewatoa hofu wakulima kuwa serikali imeliona tatizo la kushuka kwa bei na itamfidia mkulima kwa kuondoa makato ya pembejeo zote alizokopeshwa ikiwemo mbegu na viuadudu ili kuleta unafuu kwa wakulima

PICHANI: Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba akizungumza na wakulima katika sherehe za uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba

Katika msimu huu wa ununuzi 2023/24 uzalishaji wa pamba unatarajiwa kufikia tani 400,000 kulinganisha na uzalishaji wa tani 174,031 za msimu wa ununuzi 2022/23.