Habari

Imewekwa:: May, 18 2022
News Images

MSIMU WA UNUNUZI WA PAMBA 2022/23 KUANZA RASMI MEI 20 2022

Pamba ­­huchukua takribani kati ya siku 135-150 kupandwa hadi kukomaa na kuvunwa tangu kupandwa kwa mujibu wa kalenda ya kilimo cha pamba.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilitoa maelekezo kuwa Msimu wa pamba uzinduliwe mapema mara wakulima wanapoanza kuvuna pamba ili umuepushie mkulima kuuza pamba katika mifumo isiyo rasmi na kwa bei ya chini,mifumo inayofaamika kama “machinga”

Hivyo katika kuendelea kutekeleza agizo la serikali Bodi ya Pamba imeendelea kuhakikisha kuwa msimu wa ununuzi wa pamba unaanza mapema kati ya mwezi wa tano (5) au wa sita (6) kipindi ambacho maeneo mengi wakulima uanza kuvuna pamba katika kanda ya Magharibi (mikoa mingi ya kanda ya ziwa)

Msimu huu wa ununuzi 2022-2023 uzinduzi unatarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Mahaha wilayani Magu ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa watahudhuria wakiongozwa na Waziri wa kilimo Mh. Hussein Bashe (mgeni rasmi) ambaye vilevile ni mbunge wa Nzega mojawapo ya wilaya vinara uzalishaji pamba kwa mkoa wa Tabora

Wakulima wa pamba katika siku hii wanatarajia kusikia bei dira ya pamba ikitangazwa sambamba na kuanza rasmi kwa ununuzi wa pamba katika vituo vya kuuzia pamba hapa nchini. Bei dira hutoa mwelekeo wa bei ya kilo moja yap amba mbegu sokoni kwa mkulima ambapo miaka mingi imekuwa ikiongezeka kutegemea na kiwango cha ushindani katika soko

Uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba msimu huu unaenda sambamba na uzinduzi wa kampeni maalum ya kuimarisha ubora na usafi wa pamba ambapo Waziri wa Kilimo Mh. Hussein Bashe atazindua vifaa maalum vya kuvunia kwa ajili ya wakulima na vya kubebea vitakavyotumiwa na wanunuzi wa pamba

Kampeni ya ubora ni maalum ku­­­punguza tatizo la uchafuzi wa pamba kuanzia ngazi ya mkulima hadi kufika kiwanda cha kuchambulia pamba. Kufanikiwa kwa kampeni hii kutaongeza sifa za pamba ya Tanzania kimataifa na matokeo yake pamba kupata bei nzuri ambayo itamnufaisha mkulima na kuongeza pato la serikali kupitia usafirishaji nje