Habari

Imewekwa:: May, 11 2021
News Images

SERIKALI YAFUTA MADENI YA PEMBEJEO KWA WAKULIMA WA PAMBA


Wakati wakulima wa pamba maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Kanda ya Magharibi (sehemu kubwa ya Kanda ya Ziwa) wakianza shughuli za uvunaji wa pamba, siku ya Jumatatu Mei 10, 2021 wakulima wa Kijiji cha Mkula wilayani Busega mkoani Simiyu wao walikuwa wakiwakaribisha wageni wa kitaifa katika Shamrashamra za kuukaribisha msimu mpya wa ununuzi wa pamba 2021/2022 nchini

Uzunduzi huo wa Msimu wa ununuzi wa pamba ulifanywa na Mgeni Rasmi wa hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano S Mwera aliyekuwa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ulihudhuriwa na Wadau wa mbalimbali wa Tasnia ya Pamba wakiwemo wakulima, wanunuzi na wachambuaji wa pamba pamoja na wadau wengine wa maendeleo

Akiwahutubia wakulima na wananchi wa kijiji cha Mkula na wadau waliohudhuria hafla Mhe. Mwera amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan imejikita kuhakikisha inasimamia mazao ya kimkakati ikiwemo pamba ili kuhakikisha yanamnufaisha mkulima kwa kusimamia uongezaji wa tija, uhakika wa masoko ili kufikia lengo la Uchumi wa Viwanda

Aidha Mhe. Mwera alielezea changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika tasnia ambazo zikipatiwa ufumbuzi tutaweza kufikia lengo la kuwa na uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya mkulima wa pamba. Changamoto kubwa ni tija kuwa chini hali inayochangiwa na mambo mtambuka kama vile: huduma za ugani kutokuwa toshelevu, mabadiliko ya tabia nchi na tija ndogo inayosababishwa na baadhi ya wakulima (30%) kutofuata kanuni za kilimo bora cha pamba

Vilevile mgeni rasmi alitoa taarifa zilizopokelewa kwa shangwe na wakulima wa pamba baada ya kutangaza kuwaSerikali imeyafuta madeni/mikopo ya pembejeo (mbegu,viuadudu&vinyunyizi) ya msimu huu wa kilimo (Msimu wa Kilimo 2020/21) kwa wakulima wote wa pamba nchini. Badala yake madeni hayo yatalipwa na Mfuko wa Kuendeleza Zao la Pamba huku akitoa wito kwa wakulima kuendelea kujiunga na vyama vya Msingi (AMCOS) ili wawe kwenye utaratibu wa kupata pembejeo msimu unaokuja

Bei ya Pamba Msimu wa 2021-22 inatarajiwa kuwa Tshs 1,050/= kwa kilomoja ya pamba mbegu ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 (30%) kutoka bei ya shilingi 810 ya msimu uliopita wa 2020-21