Habari

Imewekwa:: Nov, 27 2020
News Images

SHEHENA YA MBEGU ZA KUPANDA ZA PAMBA YANASWA IKITOROSHWA KWENDA KUKAMULIWA MAFUTA


Mbegu za pamba kiasi cha tani 25 zilizoandaliwa kwa ajili ya wakulima wa pamba wilaya ya Busega msimu wa kilimo 2020-21 zimekutwa zimefichwa katika kiwanda cha kuchambua pamba cha Chesano kilichopo wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu ili zikiwa zimetoroshwa na kufichwa kiwandani hapo kwenda viwanda vya kukamua mafuta.

Kukamatwa kwa kiasi hicho cha mbegu chenye thamani ya shilingi milioni 16 kunafuata uchunguzi uliofanywa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ikiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Bi Tano Mwera kwa kushirikiana na TCB baada ya kupata taarifa kuwa kuna mbegu zimefichwa kiwandani hapo badala ya kupelekwa kwa wakulima kama ilivyokusudiwa.

Wilaya ya Busega inakadiriwa kutumia zaidi ya tani 400 za mbegu kwa msimu hivyo kutoroshwa kwa mbegu hizo kunakadiriwa kungeshusha uzalishaji wa pamba kwa zaidi ya 5% na kuwaathiri wakulima ambao ndio walengwa wa mbegu hizo

Katika operesheni hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Busega Bi. Tano Mwera watu watatu wanashikiriwa na jeshi la polisi wilaya ya Busega kwa kuhusika na wizi huo wenye lengo la kuhujumu juhudi za serikali katika kuwahudumia wakulima wa pamba.

Wilaya ya Busega ilizalishaji zaidi ya tani 10,000 za pamba katika msimu uliopita na pamba ni mojawapo ya mazao makuu ya biashara wilayani humo likiwakomboa wakulima kiuchumi na kuingizia mapato halmashauri.

Jumla ya tani 12,000 za mbegu za pamba zitasambazwa kwa wakulima wa pamba nchi nzima msimu wa kilimo 2020-21 na Bodi ya Pamba imejipanga zoezi hilo kukamilika mwisho wa mwezi Novemba huku upandaji wa pamba ukiwa unaendelea mikoa yote ya Kanda ya Magharibi hadi Desemba 25, 2020