TCB YAWAPA UHAKIKA WA MBEGU BORA WAKULIMA MSIMU WA KILIMO 2025/2026

SERIKALI kupitia Bodi ya Pamba, inaendelea na uchakataji na usambazaji wa mbegu bora za pamba za kupanda ikiwa ni maandalizi ya msimu wa kilimo cha pamba 2025/2026, huku ikiwaondoa hofu na kuhakikishia wakulima wa zao hilo juu ya upatikani wa Mbegu za kupanda na kuahidi kuwa kila mkulima atafikiwa na pembejeo hiyo.
Aidha, Bodi itahakikisha kunakuwa na mbegu za kutosha katika msimu wa kilimo cha pamba 2025/2026 na kuwataka wakulima kuendelea kufanya maandalizi ya mashamba ikiwemo kukata, kung'oa na kuondoa masalia ili kudhibiti kuzaliana kwa wadudu kutoka msimu mmoja kwenda mwingine ambao usababisha mashambulizi ya mapema ya mazao ya mkulima.
Msimamizi wa uchakataji wa Mbegu katika kiwanda kimojawapo cha uchakataji mbegu cha Triwin Co. Ltd kilichopo Bariadi mkoani Simiyu Bw. Ndinda Anthony ambaye pia ni Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Bariadi, amesema kuwa katika msimu huu wa kilimo 2025/2026 wanatarajia kuchakata kiasi cha mbegu Tani elfu 15 kiwandani hapo.
Amesema zoezi la upokeaji wa mbegu litafungwa wiki hii na kubakiza zoezi la uchakataji wa Mbegu ambapo hadi sasa wamechakata mbegu tani elfu 7.8 ambapo mbegu hizo zimeshaanza kupelekwa kwa Wakulima wa pamba katika wilaya mbalimbali.
"Kiwanda Cha Triwin kitasambaza mbegu za Pamba Kwa wakulima wa mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara pia kutokana na mahitaji, mbegu hiyo itasambazwa Mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine...mbegu ya msimu huu imezingatia ubora unaohitajika yaani uoataji" amesema Ndinda.
Amesema kuwa endapo mkulima akipata mbegu yenye Ubora ni moja ya sifa ya kujihakikishia mavuno na kwani mavuno ya Pamba yanaanzia kwenye ubora wa mbegu ambapo kila mbegu inayoandaliwa na Bodi ya Pamba ili kwenda kwa Wakulima inafanyiwa majaribio.
Amewataka wakulima wa Pamba katika msimu wa kilimo cha pamba 2025/2026 kuondoa wasiwasi kwani inayoandaliwa katika msimu huu inatoa kwa zaidi ya asilimia 98.
"Wakulima wa pamba wasiwe na wasiwasi mbegu ya mwaka huu inaota, serikali iko bega kwa bega na wakulima kuhakikisha kusudi la kuzalisha kwa tija linafikiwa...Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu zimeshapata mbegu na tunaongeza mbegu kulingana na mahitaji na molali wa wakulima na serikali itahakikisha kila mkulima anayelima Pamba anapata mbegu" amesema.
Msimu wa kilimo 2025/2026 uchakataji wa mbegu za kupanda unafanyika katika viwanda viwili tofauti vya Triwin Co. Ltd kilichopo Bariadi mkoani Simiyu na Jielong Holdings Ltd cha mjini Shinyanga. Aidha, viwanda hivi kwa pamoja vinatarajiwa kuchakata tani 28,000 za mbegu zenye vyuzi na jumla ya tani 25,000 zilizoondolewa nyuzi kimekanika zitazalishwa na kusambazwa kwa wakulima kwa ajili ya kupanda