WAZIRI CHONGOLO AZITAKA BODI ZA MAZAO KUIMARISHA UZALISHAJI WA KIBIASHARA NA TIJA
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo(Mb), amezitaka bodi za mazao nchini kuwa na mikakati madhubuti na endelevu ya kuongeza uzalishaji wenye tija na kuhakikisha masoko ya uhakika kwa mazao ya wakulima, ili kilimo kiwe cha kibiashara na chenye manufaa halisi kwa mkulima.
Akizungumza wakati wa kikao kazi chake na Wakurugenzi Wakuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Bodi ya Tumbaku Tanzania, Bodi ya Pamba Tanzania pamoja na Bodi ya Sukari Tanzania, Waziri Chongolo aliwahimiza viongozi hao kuandaa mikakati ya uzalishaji itakayoongeza tija, kupunguza gharama na kuboresha masoko ya mazao. Kikao hicho kimefanyika tarehe 25 Novemba 2025 jijini Dodoma, na kuhudhuriwa pia na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Sukari (NSI).
Pamba: Mbegu Bora na Kupunguza Gharama
Kwa upande wa zao la pamba, Waziri Chongolo ameielekeza Bodi ya Pamba kukaa pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa ajili ya kuandaa mikakati endelevu ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa mkulima wa pamba.
“Tusizalishe hasara, bali tija. Hatuwezi kuendelea na mazingira yale yale; ni lazima kumlinda mkulima kwa kuonesha takwimu zenye tija,” ameongeza.
Msisitizo kwa Sekta ya Sukari
Kwa upande wa sekta ya sukari, Waziri Chongolo ameielekeza Bodi ya Sukari kuanzisha mfuko maalum utakaosaidia kugharamia shughuli za uendeshaji wa Chuo cha Taifa cha Sukari, ili chuo hicho kiweze kuandaa mitaala inayoendana na ukuaji wa teknolojia ya sukari na viwanda. Aidha, bodi hiyo imeagizwa kuja na mkakati wa kuongeza uzalishaji wa sukari ili kukidhi mahitaji ya ndani na pia kuanza uzalishaji wa ethanol kibiashara.
Kahawa: Kuimarisha Uchakataji wa Awali
Kuhusu zao la kahawa, Waziri Chongolo ameitaka Bodi ya Kahawa kutoa msukumo kwa vyama vya ushirika (AMCOS) kuhakikisha vinakuwa na mashine za kutosha za kukoboa kahawa (uchakataji wa awali) na kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya ununuzi wa mashine hizo.
“Serikali na mkulima tushirikiane kwa vitendo ili kumuwezesha mkulima kuongeza tija. Hii ndiyo njia ya kuhakikisha mkulima wa kahawa ananufaika ipasavyo,” amesisitiza.
Tumbaku: Teknolojia Mbadala ya Ukaushaji
Aidha, Waziri Chongolo ameitaka Bodi ya Tumbaku kutafuta teknolojia mbadala ya kukaushia tumbaku kwa kutumia nishati ya jua (solar), hususan kutoka nchi za China au Vietnam, huku akisisitiza wataalamu kutatua changamoto zote za kiteknolojia kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji na upatikanaji wa masoko.
Kwa ujumla, Waziri Chongolo amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuona mazao ya biashara yanazalishwa kwa tija, yanapata masoko ya uhakika, na mkulima ananufaika moja kwa moja na juhudi zake kupitia uzalishaji wenye faida na ushindani.