MSIMU WA UNUNUZI WA PAMBA 2026-2027
Bodi ya Pamba Tanzania inapenda kuwatangazia wadau uzinduzi rasmi wa Msimu wa Ununuzi wa Pamba wa mwaka 2026/2027 utakaofanyika tarehe 10 Mei 2026 katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora.
Uzinduzi huu unaashiria mwanzo rasmi wa msimu wa ununuzi wa pamba na ni jukwaa muhimu litakalowakutanisha wadau wote wa pamba ikijumuisha; wakulima wa pamba, wanunuzi, wawekezaji, vyama vya ushirika, taasisi za kifedha, wadau wa kilimo pamoja na viongozi wa Serikali kwa lengo la kuendelea kuimarisha maendeleo ya sekta ya pamba nchini.
Tukio hili litaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuleta mageuzi katika sekta-ndogo ya pamba kupitia kuongeza uwekezaji, kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya zao la pamba, kuboresha upatikanaji wa masoko pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo kupitia mipango mbalimbali ya mageuzi ya sekta ya kilimo.
Aidha, kupitia uzinduzi huo, wadau watapata fursa ya:
- Kutathmini mafanikio na changamoto za msimu uliopita wa pamba;
- Kuhamasisha ununuzi wa pamba unaozingatia haki na uwazi;
- Kukuza uzalishaji na utunzaji wa pamba yenye ubora;
- Kuimarisha ushirikiano kati ya wakulima, wanunuzi na wawekezaji; na
- Kuwatia hamasa wakulima kuelekea msimu mpya wa kilimo.
Bodi ya Pamba Tanzania inawaalika wadau wote wa sekta-ndogo ya pamba pamoja na wananchi kushiriki katika tukio hili muhimu la kitaifa ili kuendelea kushirikiana katika kuboresha kipato cha mkulima wa pamba na kuongeza mchango wa sekta ya pamba katika uchumi wa Taifa.
Imetolewa na:
Bodi ya Pamba Tanzania (TCB)
Mei, 2026