MSIMU MPYA WA PAMBA BEI YAPANDA HADI SH. 1,240 KWA KILO, SERIKALI IKIAHIDI KUENDELEA KUWALINDA WAKULIMA
Mei 10, 2026 Igunga, Tabora - Tanzania
SERIKALI imetangaza rasmi kuanza kwa msimu wa ununuzi wa zao la pamba kwa mwaka 2026/2027 huku ikitangaza bei elekezi ya shilingi 1,240 kwa kilo moja ya pamba daraja A na shilingi 620 kwa pamba daraja B.
Uzinduzi huo umefanyika tarehe 10 Mei, 2026 katika Kijiji cha Mwamashimba, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa sekta ya pamba pamoja na wakulima.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Bi. Sauda Mtondoo, amesema Serikali itaendelea kusimamia mfumo wa malipo kwa wakulima wa pamba ili kuhakikisha wanalipwa kwa wakati na kwa haki.
“Msimu wa ununuzi wa pamba 2026/2027 umefunguliwa rasmi leo na bei elekezi ya kununulia pamba itakuwa shilingi 1,240 kwa kilo moja ya pamba ya daraja A na shilingi 620 kwa daraja B. Naelekeza taratibu zote zizingatiwe, wakulima walipwe kwa wakati na haki itendeke kwa kila mdau,” amesema Bi. Mtondoo.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazojitokeza katika mfumo wa ununuzi wa pamba ili kuhakikisha mkulima ananufaika ipasavyo na jasho lake.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Ndg. Renatus Luneja, amesema Bodi inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya pamba nchini, ikiwemo mpango wa kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mbegu ya pamba katika Kijiji cha Mbutu, Wilaya ya Igunga.
Luneja pia amewatahadharisha watu wanaojihusisha na udanganyifu wa mizani kuwa Serikali imeweka mifumo madhubuti ya kudhibiti vitendo hivyo.
“Mizani ya mwaka huu ikichezewa itaharibika hapohapo. Tunataka kuhakikisha mkulima anapata haki yake kwa kipimo sahihi. Malipo yatafanyika kwa njia ya fedha taslimu, simu au kupitia benki,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha ambaye alikuwa miongoni mwa wakuu wa mikoa Jirani walioshiriki uzinduzi huo, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha sekta ya kilimo kupitia Mpango wa Building a Better Tomorrow (BBT), unaolenga kuongeza maarifa na tija kwa wakulima wa pamba.
“Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan haiwezi kukubali jambo lolote linalokwenda kinyume na maslahi ya wakulima. Asilimia 70 ya pamba tunayolima huuzwa nje ya nchi huku asilimia 30 ikitumika ndani ya nchi. Serikali imetangaza bei elekezi kwa lengo la kuwalinda wakulima dhidi ya unyonyaji,” amesema Macha.
Uzinduzi wa msimu huo umebeba matumaini mapya kwa wakulima wa pamba nchini, hususan katika kuongeza kipato, kuimarisha uzalishaji wenye tija na kukuza mchango wa zao hilo katika uchumi wa taifa.