Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bodi ya Pamba Tanzania

MASALIA YA PAMBA KUWA FURSA MPYA KWA WAKULIMA KUPITIA MBOLEA YA UKAA NA BIASHARA YA KABONI “CARBON CREDIT”

Imewekwa: 08 September, 2026
MASALIA YA PAMBA KUWA FURSA MPYA KWA WAKULIMA KUPITIA MBOLEA YA UKAA NA BIASHARA YA KABONI “CARBON CREDIT”

 

Mwanza, Septemba 8, 2026

Wakulima wa pamba nchini wanatarajiwa kupata fursa mpya ya kuongeza kipato kupitia biashara ya “carbon credit, baada ya Shirika la Kimataifa la Ushauri wa Pamba (International Cotton Advisory Committee – ICAC) kuwasilisha mpango wa kutumia masalia ya pamba kuzalisha Biochar na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Mpango huo uliwasilishwa na ujumbe wa ICAC ukiongozwa na Mwanasayansi Mkuu, Dkt. Keshav, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka kampuni ya uthibitishaji wa biashara ya kaboni Merago Inc., walipotembelea ofisi za makao makuu ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) Mwanza tarehe 7 Septemba 2026, ambapo walikutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Godwin Makori pamoja na Menejimenti ya Bodi.

Akielezea mpango huo, Dkt. Keshav alisema lengo ni kuwawezesha wakulima wa pamba kushiriki katika biashara ya “carbon credit” kwa kutumia masalia ya pamba ambayo baada ya mavuno hubaki mashambani.

Alisema badala ya masalia hayo kuondolewa na kuchomwa moto, jambo linaloweza kuchangia uzalishaji wa hewa ukaa, yanaweza kukusanywa na kutumika kutengeneza mbolea ya ukaa, bidhaa inayoweza kutumika katika mashamba ya wakulima kwa ajili ya kuboresha hali na rutuba ya udongo.

Kwa mujibu wa mpango huo, matumizi ya masalia ya pamba katika uzalishaji wa Biochar yana manufaa makubwa kwa mkulima na mazingira. Mkulima atanufaika kwa kupata pembejeo inayoweza kutumika kuboresha udongo, wakati huo huo akichangia kupunguza hewa ukaa inayotokana na uchomaji wa masalia ya pamba.

Aidha, kupitia mfumo wa carbon credit, kiwango cha hewa ukaa kinachopunguzwa au kuhifadhiwa kutokana na shughuli hizo kinaweza kuthaminishwa na kuuzwa katika soko la biashara ya kaboni, hivyo kumpatia mkulima chanzo cha ziada cha kipato nje ya mapato yanayotokana na mauzo ya pamba.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Mhandisi. Godwin Makori, amepongeza ujio wa mpango huo na kueleza kuwa ni fursa muhimu inayoweza kuongeza thamani ya shughuli za kilimo cha pamba na kuboresha kipato cha wakulima na kuwapunguzia harubu ya kung’oa na kuchoma masalia ya pamba.

Mha. Makori amesema Bodi iko tayari kushirikiana na ICAC na wadau wengine katika kuhakikisha fursa hiyo inawafikia wakulima na kutekelezwa kwa manufaa ya sekta ndogo ya pamba. Ujio wa mradi wa kaboni unaendeleza juhudi ambazo tayari zimeanza kufanywa na Bodi ya Pamba Tanzania katika matumizi yenye tija ya masalia ya pamba.

 

Amesisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuanza kuona masalia ya pamba kama rasilimali yenye thamani, badala ya taka zinazopaswa kuchomwa au kutupwa, na amewataka kuchangamkia fursa hiyo mpya ya kuongeza kipato huku wakishiriki katika uhifadhi wa mazingira.

Kwa kuanzia, mpango wa carbon credit unatarajiwa kuhusisha mafunzo na utekelezaji katika wilaya za Magu, Busega, Bariadi, Meatu, Maswa, Itilima, Igunga, Kishapu na Kwimba.

Hatua hii inakuja katika kipindi ambacho wakulima wanaendelea na maandalizi ya mashamba kuelekea msimu wa kilimo wa 2026/2027, ikiwa ni pamoja na kuondoa masalia ya pamba katika mashamba.

Kupitia mradi huo, wakulima watafundishwa namna bora ya kukusanya na kutumia masalia hayo kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea ukaa, sambamba na kuelewa namna wanavyoweza kushiriki katika mfumo wa carbon credit.

slot gacor