Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bodi ya Pamba Tanzania

UWEKEZAJI KATIKA KONGANI YA VIWANDA KUCHOCHEA MAENDELEO YA TASNIA YA PAMBA NCHINI

Imewekwa: 12 September, 2026
UWEKEZAJI KATIKA KONGANI YA VIWANDA KUCHOCHEA MAENDELEO YA TASNIA YA PAMBA NCHINI

Mwanza , Septemba 11 2026

Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO), kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) na kampuni ya Birchand Oil Mills Ltd., imefanya kikao cha pamoja kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uwekezaji wa Kiwanda cha Mbolea Hai (Biofertilizer) katika Kongani ya Viwanda ya Bodi ya Pamba iliyopo wilayani Misungwi, mkoani Mwanza.

Kikao hicho kimefanyika leo katika Ofisi za Makao Makuu ya Bodi ya Pamba Tanzania na kuongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Eng. Godwin Makori.

Katika kikao hicho, ATO iliwakilishwa na Dkt. Juma Makaranga, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Sekta Binafsi, ambaye aliwasilisha Mpango wa Biashara wa Mradi wa Mbolea Hai, ukieleza fursa za uwekezaji, uendelevu wa kibiashara, mahitaji ya mtaji na mchango wa mradi katika kuongeza tija ya kilimo, kulinda mazingira na kuimarisha kipato cha wakulima.

Kwa upande wake mwekezaji kampuni ya Birchand Oil Mills Ltd ya jijini Mwanza kupitia Mtendaji Mkuu wake Wakili Leonard Sylvanus, imeeleza utayari wa kuendelea kushirikiana na taasisi za umma katika utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, kampuni hiyo imeonesha nia ya kuwekeza takribani Dola za Marekani milioni 10 (USD 10 Million) katika mradi huo, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji wa pembejeo za kilimo, kuchochea uwekezaji katika sekta ya viwanda na kuongeza tija katika uzalishaji wa pamba nchini.

Mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mnyororo wa thamani wa pamba, kuongeza matumizi ya pembejeo rafiki kwa mazingira na kujenga sekta ya pamba yenye tija, ushindani na manufaa zaidi kwa mkulima.

slot gacor