Habari

Imewekwa:: Oct, 17 2021
News Images

WAKULIMA WA PAMBA WAASWA KUTUMIA MATOKEO YA UTAFITI KUJIONGEZEA TIJA

Wakulima wa zao la pamba nchini wameshauriwa kutumia vipimo vipya wakati wa upandaji wa zao hilo ili kuweza kuwa na kilimo bora na chenye tija.

Mratibu wa zao la Pamba kutoka kituo cha utafiti Ukiliguru Dr, Paul Saidia ameleeza kuwa vipimo vipya vitaleta mabadiliko na kumuongezea mkulima idadi ya miche kutoka 22, 222 ya awali alipokuwa akitumia vipimo vya sentimeta 90 Kwa 40 na kufikia miche 444, 400 kwa kutumia vipimo vya sasa vya sentimeta 60 kwa 30

"Kwa ongezeko hili la idadi ya mimea kwa ekari mkulima atarajie kuongeza uzalishaji mara mbili ya uzalishaji wa awali ambapo ekari moja ya pamba itamwezesha kupata kilo 2000 kutoka kilo 1000 kwa ekari " alisema Dr Paul.

Dr, paul amesema kuwa kuanzia mwaka 2017 walianza utafiti kwa kushirikiana na watafiti kutoka chuo cha Lavras Brazil na kuona upandaji wa zao la pamba unaweza kubadilika na kuleta tija kwa wakulima na kuongeza kipato cha nchi.

Amesema baadhi ya Mikoa walioanza kufanyia utafiti huo ni Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga na Mara na kuweza kugundua kupitia utafiti shirikishi wa kutumia vipimo vya sentimeta 60 kwa 30 utaweza kuongeza idadi ya mimea hadi kufikia mara mbili ya vipimo vya awali.

Dr, Paul amesema kuwa mkulima atayepanda pamba kwa kuzingatia vipimo vipya vya sentimeta 60 kwa 30 na kuweza kufata kanuni zinazosimamia kilimo bora cha pamba ataweza kujiongezea kipato mara mbili ya kipato alichokuwa akipata wakati wa upandaji wa awali.

" mfano mkulima mmoja wa kishapu alikuwa anavuna kilo 200 kwa eneo la ekari moja baada ya kupata elimu ya upandaji kwa kutumia vipimo vipya mwaka huu tulipomtembelea anakilo 224 kwa eneo la robo ekari" alisema Dr, Paul.

Hata hivyo ameeleza kuwa Changamoto walizozipata baada ya kuanza kampeni ya utafiti shirikishi ni pamoja na wananchi kutokubali vipimo vipya na kueleza kuwa wamezoea upandaji wa pamba kwa kurusha.

"Kuna baadhi ya wakulima waliojitolea kushiriki katika kampeni hiyo ya utafiti shirikishi kuna wengine waliwavunja moyo kwa kuwaambia wanapoteza muda"alisema Dr, Paulo.

Aidha ametoa wito kwa wakulima kutumia vipimo hivyo vipya vya upandaji pamoja na kutumia mbolea asilia katika upandaji wa pamba kwani zao hilo linahitaji virutubisho kutoka kwenye udogo.