Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Bodi ya Pamba Tanzania

TCB NA TARI KUIMARISHA USHIRIKIANO KWA MAGEUZI YA TASNIA YA PAMBA

Imewekwa: 19 September, 2026
TCB NA TARI KUIMARISHA USHIRIKIANO KWA MAGEUZI YA TASNIA YA PAMBA

Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika tafiti za kilimo cha pamba, hususan tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na kuongeza uzalishaji na tija ya zao la pamba nchini.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Menejimenti ya Bodi ya Pamba Tanzania na TARI kilichofanyika tarehe 18 Septemba 2026 katika Ofisi za Bodi ya Pamba Tanzania, Makao Makuu, Mwanza.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Mhandisi Godwin Makori, aliishukuru na kuipongeza TARI kwa kazi kubwa inayofanywa katika kuhakikisha tafiti za kilimo zinajikita katika maeneo muhimu yanayogusa moja kwa moja uzalishaji wa pamba, ikiwemo afya ya udongo, mbegu, magonjwa ya mimea, mabadiliko ya tabianchi pamoja na matumizi ya zana na teknolojia mbalimbali za kilimo.

Mhandisi Makori alisisitiza umuhimu wa wataalamu wanaohudumia wakulima kuwa na uelewa mpana wa matokeo ya tafiti ili waweze kumsaidia mkulima kwa ufanisi na kushughulikia kwa wakati changamoto zinazowasilishwa na wakulima.

Alieleza kuwa, kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kuna umuhimu wa kuendelea kufanya tafiti za mbegu zitakazoweza kuhimili mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, sambamba na kutafuta zana rahisi za kilimo zitakazosaidia kukabiliana na changamoto ya magugu katika uzalishaji wa pamba.

“Moyo wa maendeleo ya nchi ni utafiti, lakini thamani ya utafiti inaonekana pale matokeo yake yanapomfikia mtumiaji wa mwisho na kutatua changamoto aliyonayo,” alisema Mhandisi Makori.

Aidha, Mhandisi Makori alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo mzuri wa mtiririko wa taarifa unaoanzia kwa mkulima, kufikishwa kwa watafiti na hatimaye kuwepo kwa mrejesho wa matokeo ya utafiti kwa mkulima. Mfumo huo, alisema, utasaidia kuhakikisha changamoto zinazobainishwa mashambani zinapata majibu ya kitaalamu na kwa wakati.

Katika eneo la mbegu, Mhandisi Makori alishauri kuimarishwa kwa ukaguzi katika hatua zote za uzalishaji na usambazaji wa mbegu ili kupunguza uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa ya pamba. Pia alipendekeza kufanyika kwa “survey” shirikishi za magonjwa ya pamba zitakazowahusisha wakulima na wataalamu wa utafiti ili kupata taarifa sahihi kutoka katika maeneo ya uzalishaji.

Vilevile, ametoa msisitizo kwa TCB na TARI kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kukamilisha mchakato wa usajili wa mbolea hai ya pamba inayojulikana kama “Go-Biofert”, hususan wakati Bodi ikiendelea na maandalizi ya uwekezaji wa kiwanda cha uzalishaji wa mbolea hai.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, alisema taasisi hiyo itaendelea kuimarisha tafiti zenye ubunifu na zinazozingatia maendeleo ya teknolojia kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kilimo na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wakulima.

Dkt. Bwana aliwataka wadau na watumiaji wa matokeo ya utafiti kuwasilisha maeneo ambayo wanaona yanahitaji msukumo zaidi wa tafiti ili TARI iweze kuelekeza nguvu na utaalamu katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Alisema TARI ina wataalamu zaidi ya 1,400 waliopo katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo taasisi hiyo iko tayari kufanya kazi kwa karibu na wadau wa sekta ya kilimo ili kuhakikisha utafiti unazalisha suluhisho zinazoweza kutumika na wakulima.

Dkt. Bwana pia aliipongeza na kuishukuru Bodi ya Pamba Tanzania kwa ushirikiano na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ukiriguru, hususan katika kuwezesha kifedha shughuli mbalimbali za utafiti zinazolenga kuendeleza tasnia ya pamba.

Akizungumzia suala la mbegu, Dkt. Bwana alieleza kuwa kwa sasa nchini inatumika aina moja ya mbegu ya pamba kibiashara, wakati kuna aina nyingine 17 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za utafiti. Alisema TARI itafanyia kazi pendekezo la kuwa na aina zaidi ya moja za mbegu zinazoweza kutumika kwa wakati mmoja, kulingana na mahitaji na matokeo ya tafiti.

Aidha, alieleza kuwa Gene Bank inayojengwa mkoani Arusha itakapokamilika itawezesha uhifadhi wa vinasaba na vizazi vya mbegu kwa muda mrefu, hatua ambayo itakuwa muhimu katika uhifadhi wa rasilimali za kijenetiki za mazao.

Katika matumizi ya teknolojia, Dkt. Bwana pia alieleza umuhimu wa kutafuta namna ya kutumia akili unde (Artificial Intelligence – AI) katika utambuzi wa magonjwa ya pamba, ikiwemo mnyauko fusari na magonjwa mengine, ili kurahisisha utambuzi wa changamoto na hatua za kuchukua mapema.

Katika kuhitimisha kikao hicho, viongozi hao walikubaliana kuunda kamati ndogo ya pamoja ya wataalamu kutoka TCB na TARI itakayoshughulikia masuala ya utafiti, ushauri wa kitaalamu kuhusu zao la pamba na ufuatiliaji wa utekelezaji wa tafiti.

Kamati hiyo pia itakuwa na jukumu la kusaidia kuimarisha mfumo wa mawasiliano kati ya wakulima, Bodi, watafiti na wadau wengine, pamoja na kuhakikisha matokeo ya tafiti yanafanyiwa kazi na kufikishwa kwa mkulima kama mtumiaji wa mwisho.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza kasi ya upatikanaji wa suluhisho za kisayansi na kiteknolojia kwa changamoto za uzalishaji wa pamba, kuongeza tija ya mkulima na kuchangia katika kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa pamba nchini.

 

slot gacor