TCB YAFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI “PAMBA INDUSTRIAL PARK”
Menejimenti ya Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) imefanya ziara katika eneo la kongani ya viwanda la Bodi ya Pamba “Pamba Industrial Park”, lililopo Kijiji cha Nyamatala, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, lenye ukubwa wa takribani ekari 1,000, linalotarajiwa kuwa kituo kikuu cha uwekezaji na uongezaji thamani wa zao la pamba nchini.
Ziara hiyo iliongozwa na Mkurugenzi wa Usimamizi na Udhibiti, Bw. James Shimbe, aliyemwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB Mhandisi Godwin Makori ambapo amesema Bodi imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika kongani hiyo, hususan katika viwanda vya kuongeza thamani ya pamba na uzalishaji wa pembejeo za kilimo, sambamba na kutoa fursa kwa wawekezaji wengine kushiriki katika uendelezaji wa mnyororo wa thamani wa zao la pamba.
Bw. Shimbe pia aliwasisitiza wananchi waliokuwa wakitumia eneo hilo hapo awali kupisha shughuli za uendelezaji, akieleza kuwa Serikali tayari imelipa fidia kwa wahusika ili kuwezesha matumizi ya eneo hilo kwa shughuli za maendeleo, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha mbolea hai.
Katika ziara hiyo, Menejimenti ya TCB ilifanya makabidhiano ya eneo na GESAP ENGINEERING LTD, kampuni iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa jengo litakalotumika kwa ajili ya kiwanda hicho. Akizungumza wakati wa makabidhiano, Bw. Shimbe aliitaka kampuni hiyo kuanza kazi mara moja na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, akisisitiza kuwa Serikali imeipa kampuni hiyo dhamana ya kutekeleza mradi huo.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kutoa zaidi ya ajira 500 za moja kwa moja na kuzalisha takribani lita milioni 7.5 za mbolea kwa mwaka baada ya usimikaji wa mitambo kukamilika. Mradi unatarajiwa kukamilika mwaka 2027, huku mbolea ikitarajiwa kuanza kuwafikia wakulima kuanzia msimu wa kilimo wa 2027/2028.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa GESAP ENGINEERING LTD, Mhandisi Yona Lwiva, amesema kampuni hiyo iko tayari kuanza ujenzi mara moja baada ya kukabidhiwa na kuoneshwa eneo la mradi. Aidha, ameomba ushirikiano wa TCB katika hatua mbalimbali za utekelezaji ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.