Habari

UZALISHAJI WA PAMBA WAONGEZEKA MARA DUFU KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITATU
Juhudi kubwa zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano kupitia Bodi ya Pamba zimesaidia kukuza uzalishaji na tija katika zao la pamba na hivyo kuleta msukumo mpya katika maendeleo ya sektaa ya viwanda vya nguo nchini kutokana na ongezeko la malighafi. Ili kufikia lengo la serikali kukuza uchumi wa viwanda, suala la kuongeza uzalishaji wa pamba limepewa kipaumbele kwa kuweka mikakati maalum hususan kutafiti na kuzalisha mbegu mpya za kupanda zenye tija kubwa na sifa nzuri katika usokotaji wa nyuzi na ufumaji wa nguo.
Kwa miaka mitatu sasa, tasnia ya pamba imeshuhudia maendeleo makubwa katika uzalishaji wa pamba ambapo uzalishaji umeongezeka mara dufu licha ya changamoto zilizojitokeza. Ongezeko hili limechangiwa na juhudi kubwa zilizofanywa na serikali katika ngazi zote pamoja na Bodi ya Pamba Tanzania kama msimamizi wa tasnia ya pamba. Tasnia ya pamba nchini imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika kukuza uchumi wa nchi, mkulima na kupanua biashara nchini. Zao la pamba linachangia uchumi wa zaidi ya asilimia 40% ya watanzania katika mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji, usindikaji na uzalishaji wa nguo.
Zao la pamba linazalishwa katika mikoa 17 Tanzania bara inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Mara, Tabora, Singida, Kagera, Kigoma, Katavi na Dodoma ambayo inaunda Kanda ya Magharibi; na mikoa ya Morogoro, Iringa, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Manyara inayounda kanda ya Mashariki. Takribana asilimia 99 ya pamba yote inazalishwa katika mikoa ya Kanda ya Magharibi.
Katika kipindi cha miaka minne tasania ya pamba imeshuhudia mafanikio makubwa katika kilimo na biashara ya pamba hapa nchini. Uzalishaji wa pamba umeongezeka kutoka tani 122,362 katika msimu wa 2016/17 hadi kufikia tani 348,963 katika msimu wa 2019/2020
Mikoa | Misimu | |||
2016/17 | 2017/18 | 2018/29 | 2019/2020 | |
Shinyanga | 18,062 | 14,776 | 23,156 | 44,427 |
Simiyu | 65,515 | 71,347 | 112,915 | 165,223 |
Mwanza | 4,985 | 11,739 | 17,377 | 33,196 |
Geita | 11,993 | 12,866 | 19,565 | 32,946 |
Mara | 7,557 | 6,691 | 22,624 | 20,617 |
Kagera | 658 | 984 | 1,842 | 3,051 |
Tabora | 11,797 | 12,327 | 20,213 | 31,688 |
Kigoma | 86 | 52 | 316 | 2,258 |
Singida | 783 | 1,713 | 2,536 | 5,790 |
Katavi | - | 519 | 8,583 | |
Dodoma | 49 | 37 | 344 | |
Manyara | 495 | 157 | 571 | 247 |
Morogoro | 251 | 105 | 784 | 424 |
Kilimanjaro | 139 | 16 | 117 | 47 |
Pwani | 8 | 67 | 38 | 20 |
Tanga | 11 | 40 | 104 | 97 |
Iringa | 2 | - | 10 | 5 |
Jumla Kuu | 122,362 | 132,929 | 222,725 | 348,963 |
UZALISHAJI WA MBEGU BORA ZA KUPANDA
Ongezeko la uzalishaji limechangiwa na sababu mbalimbali kubwa ikiwa ni matumizi ya mbegu bora zenye sifa zinazostahili. Kwa zaidi ya miongo miwili tasnia ya pamba imekuwa ikitumia aina moja ya mbegu iliyofahamika kama UK91. Mbegu inapotumika kwa muda mrefu sifa zake hususan ukinzan na wadudu na tija vinapungua sana hivyo kuathiri uzalishaji. Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na wadau wengine imesimamia uzalishaji wa mbegu bora za kupanda aina ya UKM08 ambayo inatoa mavuno mengi kwa eneo na kuwa na vigezo vingi vinavyotakiwa na wazalishaji wa nguo ukilinganisha na mbegu aina ya UK91. Kwa kuzingatia umuhimu wa mbegu za kupanda, Bodi ya Pamba imesimamia uzalishaji wa mbegu kwa misimu miwili na msimu wa tatu ambao 2018/2019 wakulima wote nchini walianza kutumia mbegu mpya aina ya UKM08.
Mbegu UKM08 iliyotolewa mwaka 2008, ina sifa mbalimbali ambazo ni pamoja na mavuno ya kati ya kilo 1,000 hadi 1,200 kwa ekari, kuvumilia magonjwa hasa mnyauko fuzari (fusarium wilt), wororo wa nyuzi 4.03, urefu wa nyuzi inchi 1.275, asilimia ya nyuzi 42.3 na ugumu wa nyuzi 30.2g/tex. Mkulima wa pamba ananufaika na wingi wa mavuno kwa eneo wakati mnunuzi anafaidika na uwiano mkubwa wa nyuzi dhidi ya mbegu na msokotaji wa nyuzi na mwenye kiwanda cha nguo anaufufaika na wororo wa nyuzi pamoja na ugumu wa nyuzi wakati wa usokotaji.
Mfumo wa uzalishaji wa mbegu uliokuwa umezorota tangu kuanza kwa soko huru kwenye tasnia ya pamba mwanzoni kwa miaka 1990 ulifufuliwa kwa kuteua maeneo maalum kwa ajili ya kuzalisha mbegu za pamba za kupanda. Maeneo yaliyoteuliwa ni Shamba la Taasisi ya Utafiti (TARI) Ukiriguru lililoko Misungwi kwa ajlli ya kuzalisha mbegu mama, mbegu inayotoka Misungwi inazalishwa zaidi katika eneo teuzi katika wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi; na hatua ya mwisho katika uzalishaji wa mbegu ni mbegu kutoka Tanganyika inapelekwa wilaya ya Igunga kuzalishwa kwa ajili ya wakulima wote nchini. Maeneo yote ya uzalishaji mbegu yalikaguliwa na Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) na kuthibitika kutokuwa na magonjwa hatari (mfano mnyauko fuzari).
Wakulima wanaozalisha pamba ya mbegu walipatiwa mafunzo maalum ya jinsi pamba ya mbegu inayotakiwa kutunzwa. Huduma za ugani katika eneo la uzalishaji mbegu ziliongezwa kwa ajiri maafisa ugani maalum kipindi cha msimu wa kilimo waliokuwa wanawafikia wakulima kwa karibu, pembejeo zilikuwa zinapatikana wakati wote wa msimu na wakati wa kuuza, wakulima walipewa bei ya nyongeza kama motisha.Bodi ya Pamba ilifanya uhamasishaji mkubwa wa kuhakikisha wakulima wanazingatia kanuni kumi za kilimo bora cha pamba hasa upandaji wa pamba kwa mistari.
KUIMARIKA KWA MFUMO WA UPATIKANAJI NA USAMBAZAJI WA VIUADUDU
Ili uzalishaji, tija na ubora wa pamba viimarike suala la upatikanaji wa pembejeo ni la msingi sana; pamba isiponyunyiziwa kikamilifumkulima anaweza kupoteza hadi asilimia 80 ya mavuno. Katika misimu mitatu iliyopita matumizi ya viuadudu yameongezeka kutoka chupa (acre packs) milioni mbili kwa msimu hadi kufikia chupa milini sita msimu uliopita wa 2018/2019. Matumizi yaliongezeka sana kutokana na kuongezeka kwa wadudu kunakosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi, wakulima kujua umuhimu wa viuadudu katika zao la pamba, na kupanuka kwa eneo la uzalishaji kutoka mikoa 15 hadi kufikia mikoa 17 nchini.
KUIMARIKA KWA HUDUMA ZA UGANI.
MATUMIZI YA KAMBA ZA KUPANDIA.
Ili kuwezesha wakulima kupandapamba kitaalam na kuwa na kwa nafasi inayopendekezwa na wataalam, Bodi ya Pamba ilisambaza takriban kamba laki tatu (300,000) kwa wakulima wa pamba nchi nzima hivyo kusaidia wakulima wengi kupanda pamba kitaalam. Suala la tija ndogo kwenye uzalishaji wa pamba linachangiwa pia na upandaji holela wa pamba. Pamba inapandwa kwa nafasi ya sentimita 30 kutoka shimo (shina) moja na jingine , nafasi kati ya mstari na mstari ni sentimita 90. Mkulima akipanda kwa kuzingatia kununi hii, ekari moja inakuwa na miche isiyopugua 22,200 itakayomhakikishia mavuno ya hadi kilo 1,200.
KUIMARIKA KWA MFUMO WA UNUNUZI WA PAMBA
Pamoja na changamoto zilizojitokeza katika ununuzi wa pamba kupitia vya vya ushirika vya msingi - AMCOS, kufufuliwa kwa ushirikakumesaidi kuwakusanya wakulima pamoja na kupunguza wizi uliokuwa unafanywa na mawakala wa ununuzi wa pamba vijijini. Kampuni za ununuzi wa pamba zinapaswa kununua pamba kupitia vyama vya msingi (AMCOS); AMCOS zinakusanya pamba kutoka kwa wanachama wake ambao ni wakulima wa pamba, na pamba hiyo kuuzwa kwa kampuni itakayokuwa imeingia mkataba na AMCOS husika.
Kuunganishwa kwa wakulima katika AMCOS kumerahisisha zoezi la usambazaji wa pembejeo kwa wakulima kwa sababu viongozi wa ushirika wanawafahamu wanachama wao ambao ni wakulima pamoja na mahitaji ya pembejeo (mbegu na viuadudu).
Ukusanyaji wa takwimu pia umeimarika kwa kuwa kila shughuli inayomhusu mkulima ilinafanyika kupita AMCOS. Kwa yeyote anayehitaji takwimu za idadi ya wakulima, kiasi cha pamba kilichonunuliwa, mahitaji na matumizi ya pembejeo kwa eneo Fulani anaweza kuzipata kwenye AMCOS bila usumbufu wowote. Changamoto kubwa inayoukabili ushirika ni ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu uendeshaji wa ushirika na sheria zinazosimamia ushirika. Ni matarajio yetu kuwa Mrajisi wa Ushirika nchini ataongeza nguvu katika kutoa elimu ya ushirika kwa viongozi waliochaguliwa kusimamia AMCOS ili dosari zilizojitokeza katika miaka miwili ya uendeshaji wa ushirika kwenye tasnia ya pamba zipatiwe ufumbuzi wa kudumu
KUIMARIKA KWA ELIMU YA UGANI
Suala la elimu ya kilimo bora kwa wakulima limepewa msisitizo sana katika miaka mitatu iliyopita. Njia mbalimbali zilitumika kuwafikia wakulima ikiwa ni pamoja na mashamba darasa ambapo wakulima wanapatiwa elimu kupitia shamba la mfano linaloanzishwa katika ngazi ya kijiji au kitongoji.
Kila hatua ya uhudumiaji wa shamba inaanzia kwenye shamba darasa ili wakulima wafundishwekanuni inayotekelezwa kwa wakati huo ili iwe rahisi kwao kutekeleza katika mashamba yao.
Wakulima pia walifikiwa kwa njia ya sinema zinazoonesha utekelezaji wa kanuni kumi za kilimo bora cha pamba.
Aidha redio za jamii (community radios) zilitumika sana kufikisha elimu kwa wakulima, vipeperushi pia vilisambazwa kwawakulima vinavyoelezea kwa kina jinsi ya kuzingatia kanuni na manufaa yake. Aidha kwa kushirikiana na TARI Ukiriguru wakulima walifundishwa jinsi ya kutumia viuadudu vya pamba pamoja na vinyunyizi (mabomba) kwa ufanisi.
CHANGAMOTO ZINAZOKABILI TASNIA YA PAMBA
Licha ya mafanikio makubwa ambayo tasnia ya pamba imeyafikia katika kipindi hiki cha miaka mitatu hususan kuongezeka kwa uzalishaji na tija, bado tasnia inasumbuliwa na changamoto mablimbali ambazo ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa; mabadiliko ya mara kwa mara ya bei ya pamba katika soko la kimataifa, wakulima kukosa mikopo katika vyombo vya fedha. Mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa kikwazo kiubwa katika uzalishaji hasa unapotokea ukame wa muda mrefu pamba inshindwa kukua na pamba inayojitahidi kutoa vitumba vinapasuka mapema kabla ya nyuzi kukomaa; mvua zikiwa nyingi sana pamba inarefuka sana na haitoi matunda (vitumba).
Kutokana na Tanzania kuwa mzalisahi mdogo wa pamba duniani imekuwa mpkeaji wa bei na haina uamuzi wowote katika masuala ya bei katika soko la dunia. Asilimia kubwa ya pamba inayozalishwa nchini inauzwa ikiwa ghafi hivyo kuathiriwa sana na kuporomoka kwa bei katika soko la dunia. Lakini serikali ya awamu ya tano inalitafutia ufumbuzi suala la bei ya pamba kwa kujenga viwanda vingi vitakavyotumia pamba inayozalishwa. Mkakati wa kuongeza thamani ya pamba yetu kutaifanya Tanzania kuacha kuwa soko la malighafi na badala yake kusafirisha nguo na bidhaa nyingine nje ya nchi.
Mkakati wa serikali kufufua na kuimarisha ushirika nchini utasaidia wakulima kuwa na umoja na uwezo wa kukopa pembejeo kupitia AMCOS na kulipiahuduma hizo wakati wa kuuza pamba