Habari

Imewekwa:: Dec, 10 2021
News Images

MIAKA 60 YA UHURU NA TASNIA YA PAMBA IMARA

Katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, zao la pamba limeongezeka na kuenea katika Zaidi ya nusu ya mikoa yote Tanzania bara, ambapo takriban asilimia 40 ya watanzania hunufaika na zao la pamba katika mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji, ununuzi, uchambuaji, usafirishaji, mauzo nje ya nchi na uzalishaji wa nguo hapa nchini. Zao la pamba liliingizwa nchini Tanzania na wakoloni mwanzoni mwa karne ya 20 na kuanza kulimwa katika mikoa ya Kanda ya Mashariki ambayo ni Morogoro, Pwani na Tanga. Uzalishaji wa kibiashara ulianza miaka 1930 na ndipo viwanda vya kuchambua pamba vilipoanza kujengwa maeneo tofauti nchini.Zao la pamba lilioanza kulimwa katika mikoa mitatu ya ukanda wa mashariki lakini kwa sasa pamba inalimwa katika mikoa 17 ya Tanzania ikijumuisha Kanda ya Mashariki na Magharibi. Mikoa inayolima pamba ni pamoja na Mwanza, Geita, Simiyu, Mara, Shinyanga, Tabora, Singida, Katavi, Kagera, Kigoma, Dodoma, Manyara, Morogoro, Tanga, Iringa, Kilimanjaro na Pwani.

Bodi kama msimamizi wa tasnia ya pamba ilianzishwa miaka tisa (9)kabla ya uhuru mwaka 1952. Kwa sasa ina miaka 69. Bodi ya pamba ya kwanza ilianzishwa kwa malengo mahususi ya kukuza na kuendeleza tasnia ya pamba; kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo, kununua na kuchambua pamba na kuuza pamba nje ya nchi. Kabla ya kuanzishwa kwa Bodi ya Pamnba Tanganyika (LSMBT), pamba yote iliyozalishwa nchini ilisafirishwa kwenda nchi za nje kupitia nchini Uganda chini ya Vctoria Federation.

Baada ya uhuru, Tanganyika huru ilianza jitihada za kukuza uchumi kwa kujenga viwanda vya nguo ambavyo vilianza kutumia malighali inayotokana na pamba kutengeneza nguo. Kabla ya uhuru pamba yote iliuzwa nje ya nchi kama malighafi kuendeleza viwanda na uchumi wa wakoloni; serikali ya Tanganyika ilijenga viwanda kama Urafiki, Sungura Textile, Kiltex, Mwatex n.k ambavyo vilianza kutumia malighali zetu kuzalisha nguo na kutoa ajira kwa wananchi wa Tanganyika huru.

Kutokana na juhudi zilizofanywa na serikali kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba Tanganyika; uzalishaji uliongezeka kwa kasi na idadi ya wakulima kuongezeka ambapo hadi kufikia mwaka 1967 uzalishaji wa pamba ulifikia tani 236,802 za pamba mbegu kutoka tani 93,844 kabla ya uhuru. Hali hii ilichangiwa na usimamizi madhubuti wa Bodi chin ya serikali ya kizalendo ya Tanganyika huru. Ili kuimarisha usimamamizi wa zao mwaka 1971, Bodi ya Pamba Tanganyika ilivunjwa na kuanzishwa Mamlaka ya Pamba Tanzania. Mamlaka ya pamba ilikuwa na wajibu wa kutoa huduma za ugani kwa wakulima, kununua pamba ya wakulima, kuchambua pamba,, kuuza pamba nje ya nchi na kununua na kusambaza pembejeo kwa wakulima.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990 serikali ya Tanzania iliingia kwenye mpango wa mabadiliko ya uchumi (economic reforms and structural adjustment) kwa lengo la kukukza biashara na sekta binafsi na wakati huohio seriksli kujiondoa katika biashara na kuwa na jukumu la kusimamia sharia na kanni na kujenga mazingira rafiki kwa sekta binafsi kuwekeza katika sekta za uchumi. Sera ya soko huru iliingia rasmi kwenye zao la pamba hivyo Bodi ya Pamba ikabadilishiwa majukumu kutoka yale ya kibiashara na kuwa taasisi ya serikali inayosimamia sera na kanuni za uzalishaji, biashara na masoko ya pamba kwa noaba ya serikali.

Sekta ya pamba imeendelea kukua kwa kasi katika eneo la viwanda vya kuchambua pamba na kuongezeka kwa kampuni zinazofanya biashara ya pamba nchini. Wakati tasnia ya pamba inaongoa kwenye sera ya soko huru, kulikuwa na viwanda visibyozidi 20 vya kuchambua pamba; viwanda vilikuwa vya vyama vya ushirika na vilikuwa vinatumia teknolpjia ya kizamani. Wakati tunasherekea miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika, viwanda kuchambua pamba vimeongezekakutoka viwanda 20 hadi kufikia viwanda 80 na vimesambaa katika takriban asilimia 90 ya mikoa inayozalisha pamba. Aidha jumla ya kampuni 30 zinajihusisha na biashara ya pamba hususan ununuzi wa pamba mbegu, uchambuaji na mauzo ya pamba nyuzi nchi za nje.

Wakati taifa linaingia katika miaka 60 ya uhuru tasnia ya pamba imeimarika zaidi, viwanda vimeongezeka, idadi ya wakulima imeongezeka na kuongezeka kwa uzalishaji hadi kufikia takriban tani 376,591. Aidha mikakati ya kuhakikisha tasnia inafikia lengo la kuzalisha tani 1,000,000 za pamba katika miaka mitano ijayo zinaendelea. Mikakati hiyo ni pamoja na kuimarishwa kwa mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za pamba, kuimarisha huduma za ugani, kuimarishwa kwa elimu ya kilimo bora cha pamba na kujenga mazingira rafiki kwa sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika za la pamba.