Habari

Imewekwa:: Jul, 06 2020
News Images

Waziri ya Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) amesema serikali haitajihusisha na utaratibu wa kupanga bei za mazao ikiwemo pamba bali nguvu ya soko itatumika kuamua bei ya mazao hayo kwa mkulima. Waziri Hasunga aliyasema hayo kwenye mkutano wa wadau wa pamba uliofanyika jijini Mwanza tarehe 7/6/2020 kujadili maendeleo ya tasnia ya pamba na mkakati wa kuanza kwa msimu mpya wa ununuzi wa pamba 2020/2021.

Akifafanua maendeleo ya tasnia ya pamba kwa msimu uliopita, waziri Hasunga alisema, Uzalishaji wa pamba nchini umeongezeka kwa asilimia 185 kutoka tani 122,178 msimu wa 2015/16 hadi tani 348,910 smu wa 2019/20 tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani. “Ninawapongeza sanaWadau wa Pamba kwa ushirikiano mlioipatia Serikali kufanikisha mabadiliko makubwa katika kilimo cha pamba. Tumeshuhudia kanuni za kilimo cha pamba zikizingatiwa na kwamba wakulima sasa wanapanda kwa mistari na hivyo kuongeza tija ya pamba. Ni dhamira ya Serikali kuweka mfumo endelevu wa kilimo cha pamba ili tuweze kuzalisha kilo 1,000 kwa ekari badala ya kilo 200 za sasa” alisema Hasunga.

Changamoto nyingi ziliikumba tasnia ya pamba msimu uliopita kubwa ikiwa ni kuyumba kwa bei katika soko la dunia, hali hii iliathiri biashara ya pamba nchini na kuchelewesha mauzo na malipo ya pamba.

“Soko la dunia katika msimu wa ununuzi wa mwaka 2019/20 liliyumba na kusababisha mtikisiko ambao ulitusumbua kwa kipindi kirefu. Tulikaa vikao na Mhe. Waziri Mkuu vipatavyo 8 na hatimaye suluhisho la pamba ya wakulima kununuliwa likapatikana. Hata hivyo, baada ya msimu kumalizika baadhi ya changamoto zinaendelea kupatiwa ufumbuzi ambazo ni pamoja na na madai ya wakulima ya takriban shilini bilioni 4.6, ushuru wa Halmashauri za wilaya, AMCOS na Vyama vikuu vya ushirika (UNION)”.alisema Hangunga na kuongeza kuwa kutokana na changamoto zilizojitokeza katika mauzo na bei ya pamba kwa mkulima msimu uliopita wa 2019/2020, serikali imejifunza kwamba kupanga bei ambayo haina uhalisia wa bei katika soko la dunia hakuleti tu usumbufu kwa wakulima bali pia kunarudisha nyuma maendeleo ya tasnia, alisema Hasunga na kuongeza kwamba, wakati serikaliinaendelea na majukumu yake ya kuweka mazingira rafiki ya kibiasharayanayozingatia sheria, kanuni na taratibu, bei ya pamba itategemea hali ya soko la dunia.

Akielezea mchango wa kilimo katika kukuza uchumi na pato la nchi, Waziri Hasunga alisema kilimo kinatoa ajira kwa takriban asilimia 58 ya watanzania wote katika mnyororo wa thamani wakati asilimia 65 ya viwanda vyote nchini vinatumia malighafi zinazotokana na kilimo hivyo ipo haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kukuza na kuendeleza kilimo kwa sababu ndiyo sekta inayotegemewa kwa asilimia kubwa na watanzania kwa ajira, chakula na kipato.

Wakati tunajivunia ongezeko la uzalishaji wa chakula msimu huu kwa zaidi ya asilimia 300 msimu uliopita, uzalishaji unatarajiwa kushuka kwa kiwango kikubwa sana kutoka takriban tani 348,000 hadi tani 150,000 kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za muda mrefu. Pamoja na kushuka kwa uzalishaji wa pamba nchini, uzalishaji katika mataifa mengine hususan China ni mkubwa hivyo kuleta atahri katika suala la bei ya pamba duniani.

Wakati mahitaji ya pamba duniani ni tani milioni 24 kwa msimu, uzalishaji mwaka huu unakadiriwa kuwa tani milioni 26, na salio na mwaka jana ni tani milioni 16. Kutokana na hali hii bei ya pamba imeshuka kutoka senti 62 za Kimarekani kwa ratili msimu uliopita hadi senti 56 msimu huu, hali amabyo inatarajiwa kuathiri kwa kiwango kikubwa bei ya pamba kwa mkulima wa pamba nchini.

Akifafanua mkakati wa muda mrefu wa kuboresha bei ya pamba nchini, mhe. Hasunga alisema kwamba ni lazima kama taifa tuondokane na utaratibu wa kuuza malighafi na kuanza kuzalisha nguo kwa kutumia pamba yetu. Asilimia takriban 70 inasafirishwa nje ya nchi ikiwa ghafi na watanzania kuletewa bidhaa ikiwa ni pamoja na mitumba. Waziri wa Kilimo alisema hakuna sababu ya kuagiza sare za shule, majeshi na vifaa tiba kutoka nje ya nchi wakati tunzalisha pamba ambayo ingetumika kutengeza vifaa hivyo. Akifafanua kuhusu mkakati wa kufufua viwanda vya nguo, naibu waziri wa Biashara na Viwanda Mhe. Stella Manyanya (Mb) alisema serikali imeunda kamati maalum ambayo inafatilia ubinafsishaji wa viwanda vya nguo nje ili kuona jinsi gani ya kuviendeleza.

Akifafanua kuhusu mfumo wa ununuzi, waziri alisema kuwa ununuzi wa pamba utaendelea kufanyika kupitia AMCOS na kampuni za ununuzi zinawajibika kuzingatia utaratibu huo; lakini kuna tatizo kubwa la kukosekana uwazi katika suala la upimaji wa pamba katika AMCOS hasa katika vifaa vinavyotumika kupimia pamba. waziri aliagiza Bodi ya Pamba na wanunuzi kuhakikisha kuna kuwa n vifaa maalum vya kupimia pamba ili mkulima asiendelee kukatwa kilo moja kwa shuka linalofungia pamba wakati wa kupima. Aidha wapimaji wa pamba kwenye AMCOS wanaharibu mizani kwa lengo la kupunja wakulima hali kadhalika mizani za viwandani inakuwa na matatizo kutokana na kuwa na tofauti ya uzito wa pamba iliyopimwa kituoni na ule unaopimwa kiwandani.