Habari

Imewekwa:: Dec, 19 2018
News Images

MIKAKATI YA KUBORESHA UZALISHAJI WA PAMBA KWA MSIMU WA KILIMO 2018/2019.

Msimu wa kilimo wa 2018/19 ulianza rasmi tarehe 15/11/2018 kwa wakulima kuanza kupanda pamba katika mashamba yao. Aidha maandalizi ya msimu yalianza mwanzoni mwa mwezi Septembambegu za kupanda zilipoanza kusambazwa kwa wakulima. Kwa kuzingatia umuhimu wa zao la pamba katika maendeleo ya viwanda vya nguo nchini na uchumi wa mkulima mmoja mmoja, Bodi ya Pamba imesimamia kwa karibu kuhakikisha wakulima wote wamepata mbegu za kutosha za kupanda. Msimu huu kumekuwa na ongezeko la matumizi ya mbegu kwa takriban asilimia 25. Bodi ya Pamba na wadau wa pamba wamekuwa na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha uzalishaji wa pamba unaimarika; mikakati hiyo ni pamoja na;

  • 1.Uzalishaji wa mbegu bora

Bodi ya Pamba inaendelea kusimamia uzalishaji wa mbegu bora aina ya UKM08 ili kuhakikisha mbegu zinazozalishwa kwa viwango vinavyokidhi matarajio ya wakulima. Katika msimu wa kilimo wa 2018/19 wakulima wote wa pamba nchini watapanda mbegu mpya ya UKM08 ambayo ina tija kubwa.

Maeneo yaliyoteuliwa kwa uzalishaji wa mbegu ni shamba la Nkanziga lililoko wilaya ya Misungwi linalosimamiwa na Kituo cha Utafiti Ukiriguru, Kata ya Mwabusalu wilaya ya Meatu na wilaya yote ya Igunga. Wakulima wa maeneo haya ndiyo wanaozalisha mbegu za kupanda kwa mfumo uliokubalika. Mbegu inayotoka Nkanziga inapelekwa kwa wakulima wa Meatu ambao wanaizalisha kwa wingi kabla ya kupelekwa Igunga ambako inazalishwa kwa wingi zaidi. Mbegu zinazotoka Igunga ndizo zinazosambazwa kwa wakulima wa maeneo mengine na haitarudi tena kwa wakulima.Nkanziga, Meatu na Igunga ndiyo vitalu vya uzalishaji wa mbegu za pamba za kupanda.

2. Kusambaza kamba za kupandia kwa wakulima.

Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya zao la pamba wameweka mkakati wa kuhakikisha kuwa kila mkulima anapanda pamba kwa kutumia vipimo maalum kama inavyoshauriwa na wataalam kwa kusambaza kamba za kupandia kwa wakulima.

Msimu wa kilimo 2017/18, Bodi ilisambaza kamba zilizoandaliwa maalum kwa ajili ya kurahisisha zoezi la upandaji wa pamba kwa mistari kwenye takriban wilaya kumi na tatu (13) katika Kanda ya Magharibi na msimu wa kilimo wa 2018/19 wakulima wote watapatiwa kamba. Wakulima wakipanda pamba kwa nafasi inayopendekezwa ya sentimita 40 kutoka mche hadi mche na sentimia 90 kutoka mstari mmoja hadi mwingine, shamba litakuwa na mimea ya kutosha ambayo ni zaidi ya miche 22,000 itakayomhakikshia mkulima tija kubwa

3. Kuimarisha elimu ya matumizi ya viuadudu

Katika msimu wa kilimo wa 2018/19, mfumo wa unyunyiziaji wa viuadudu kwenye pamba utakuwa katika hatua tatu ili kukabiliana na wadudu wanaofyonza na wanaotafuna majani na matunda ya pamba na kupunguza usgugu wa viuadudu unaosababishwa na matumizi ya aina moja ya kiuadudu.

Wakulima watafundishwa namna bora ya kutumia viuadudu kwa kutumia njia mbalimbali ambazo ni pamoja na radio, sinema, mashamba darasa na mikutano ya hadhara. Aidha wakulima watafundishwa mbinu za kutega wadudu aina ya viwavi jeshi vamizi ili kudhibiti mashambulizi ya wadudu hawa hatari.

4. Kuimarisha huduma za ugani

Ili kuwafikia wakulima wengi zaidi Bodi ya Pamba itawatumia wakulima wawezeshaji waliko vijijini kutoa elimu ya kilimo bora cha pamba kwa kushirikiana na maafisa ugani. Utaratibu huu utapunguza tatizo la uhaba wa waganikatika maeneo yanayozalisha pamba.

5. Pembejeo kusambazwa kupitia Ushirika

Pembejeo zote za pamba msimu wa kilimo 2018/19 zitasambazwa kwa wakulima kupitia AMCOS ili kuhakikisha wakulima wanapata huduma kwa usahihi. Pembejeo zote zitasambazwa kwa wakulima kwa mkopo na wakulima wote wanatakiwa wajisajili na kuwa wanachama wa vyama vya msingi katika maeneo yao. Hadi kufikia tarehe 15/12/2018 zaidi ya tani 20,000 mbegu aina ya UKM08 zilikuwa zimeshasambazwa kwa wakulima kupitia AMCOS. Aidha viuadudu vyote vitasambazwa kupitia vyama vya ushirika (AMCOS)