Habari

Imewekwa:: Jul, 27 2021
News Images

SERIKALI KUPITIA BODI YA PAMBA YAJA NA MIPANGO MAHUSUSI YA KUONGEZA TIJA KATIKA KILIMO CHA PAMBA

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba imeandaa mikakati mahsusi ya kuongeza tija na uzalishaji wa zao la pamba. Katika mikakati hiyo, Bodi imelenga kukuza uzalishaji kutoka wastani wa tani 300,000 hadi kufikia tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2025. Mkakati wa kuongeza tija na uzalishaji wa pamba ulizinduliwa na Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda (MB) Waziri wa Kilimo, tarehe 4 Julai 2021 katika kijiji cha Kijeleshi wilaya ya Busega mkoani Simiyu.

Akizinduka Mkakati huo, Waziri alisema ni wakati sasa wakulima wazingatie kanuni za kilimo bora cha pamba kama sheria inavyotaka; na hili tumejipanga kulisimamia ili kupunguza umasikini. “Hii ni kampeni ya kuhakikisha wakulima wanapata faida katika kilimo cha pamba” alisema Prof. Mkenda na kuongeza kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, imelenga kuongeza uzalishaji wa pamba hadi kufikia tani milioni moja ifikapo mwaka 2025, na hili linawezekana kama wadau tukilisimamia. Waziri aliipongeza Bodi ya Pamba kwa kuja na mkakati wa kuongeza tija katika zao la pamba kwani ni hatua ya kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo.

Tangu uzalishaji wa pamba uanze hapa nchini mwanzoni mwa karne 20, uzalishaji wa juu kabisa ulifikiwa msimu wa 2005/2006 ambapo jumla ya tani 376,000 sawa na marobota 700,000 ilizalishwa.Kiwango hiki cha uzalishaji hakijafikiwa au kuvukwa kwa muongo mmoja na nusu uliopita. Uzalishaji umeendelea kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kutozingatia kanuni kumi za kilimo bora cha pamba; msimu uliopita uzalishaji ulishuka hadi kufikia takriban tani 122,000.

Mataifa mengi duniani mfano Misri wanazalisha kilo 2000 kwa ekari, Tanzania tunazalisha kilo 300. Hali hii si nzuri ni lazima ibadilike kama tunataka kuleta maendeleo endelevu kwa mkulima mmoja mmoja na taifa. “kwa sasa wakulima wanajitahidi sana kuongeza tija na uzalishaji kwa kupanua eneo la uzalishaji; lakini tukiendelea na hali hii itafika mahali eneo la kupanua litaisha” alisema Mkenda na kushauri kuwa, wakati umefika wa kutumia teknolojia katika kuongeza uzalishaji katika eneo dogo. “tunataka Simiyu itoke kwenye uzalishaji wa tani 150,000 hadi kufikia tani 500,000” alisema Prof. Mkenda na kufafanua kuwa katika mkakati huu, huduma za ugani zitaimarishwa katika mikoa yote inayozalisha pamba, kwa kuwapatia vyombo vya usafiri, vifaa vya kupima hali ya udongo pamoja na fedha za mafuta.

Waziri aliwashauri wakulima kuacha kutumia bei kama kigezo muhimu cha kuongeza uzalishaji ama kulima pamba.Msimu wa 2021/2022 bei ya pamba imeendelea kuongezeka kwa sababu, bei katika soko la dunia imekuwa nzuri kutokana na kupungua kwa wingi wa pamba katika soko la dunia, lakini hiki kisiwe kigezo cha kuwafanya mlime pamba msimu ujao; zalisha pamba kibiashara kwa kuongeza tija katika eneo dogo ambayo itakupa faida hata kama bei itashuka. Aidha utaratibu wa kudhani ili uzalishe kwa wingi ni lazima kupanua eneo siyo utaratibu mzuri kwa sababu wakati utafika eneo la kuongeza litakuwa halipo. “Ongeza tija kwenye eneo kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora cha pamba, tumia mbolea ya samadi na viwandani pamoja na ushauri wa kitaalam kutoka kwa maafisa ugani”

Teknolojia rahisi zinazobuniwa kila mara katika vituo vya utafiti ni muhimu sana zisambazwe kwa wakulima ili kuboresha kilimo. TARI Ukiriguruwamefanya utafiti wa mbinu za kuongeza tija kwa muda mrefu na kugundua kuwa nafasi ya kupandia pamba ina uwezo wa kuogeza tija.Panda pamba kwa nafasi ya futi moja kati ya mashimo na futi mbili kati ya mistari, tumia mbolea ya samadi na viwanda kuongeza wingi wa mazao na ubora” alisema Dkt Heneriko Kulembeka, kaimu Mkurugenzi TARI Ukiriguru na kuongeza kuwa nafasi ya upandaji iliyokuwa inatumika awali ilichangia mavuno kidogo kwa eneo hali iliyolazimu kufanya utafiti wa nafasi mpya ambayo imezinduliwa leo na itaanza kutumika msimu ujao wa kilimo.

Akifafanua kuhusu tatizo la tija ndogo katika kilimo cha pamba, Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Pamba ndugu Marco Mtunga alisema, umaskini wa wakulima wa pamba hausababishwi na ukosefu wa nguvukazi bali na tija ndogo inayotokana na kutokuzingatia kanuni za kilimo bora. Alisema wanatumia nguvu nyingi bila maarifa hivyo kuwafanya wakulima mara nyingi kulalamikia bei ndogo ya pamba. “Bila kutatua tatizo la tija ndogo, hata bei ikipanda maradufu, bado umaskini hautaondoka; uzalishaji wa kilo 300 kwa ekari ni mdogo sana. “ Ili kuleta chachu ya mabadiliko katika zao la pamba, wizara imemteua Ndugu Agrey Mwanri kuwa Balozi wa zao la Pamba, kwa kutambua mchango mkubwa aliotoa wakati kitalu cha kuzalisha mbegu za pamba kilipoanzishwa wilayani Igunga huku yeye akiwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora. Kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba, Balozi wa pamba atahamasisha uzingatiaji wa kanuni za kilimo bora cha zao la pamba na kuanzia mwezi Julai hadi novemba 2021”. Alisema Mtunga

Ulipowadia wasaa wa kuonesha kile ambacho wakulima wanatakiwa kukifanya ili kuongeza tija, balozi wa pamba, ndugu Agrey Mwanri alisema, kilimo chetu ni duni kisicho na faida, si cha kibiashara bali shughuli ya kujikimu. Wakulima hawako kibiashara kwa sababu wanapanda pamba hovyo bila kuzingatia vipimo “tupa mbegu tukutane wakati wa palizi”. TARI wamekuja na vipimo vipya vya kupandia pamba kwa lengo la kuongeza idadi ya mimea kwa eneo, kwa vipimo vipya vya futi moja shimo hadi shimo na futi mbili mstari hadi mstari mkulima atakuwa na uwezo kwa kuongeza uzaishaji mara mbili. Vipimo vya zamani vilimpatia mkulima mimea 22,222 kwa ekari wakati vipimo vipya itakuwa mimea 44,444. Idadi ya mimea ni hatua ya kwanza ya kuboresha tija.