Habari

Imewekwa:: May, 17 2021
News Images

MSIMU WA UNUNUZI WA PAMBA 2021/2022 WAZINDULIWA

Bei ya pamba 1,050/kg

Madeni ya pembejeo kwa wakulima yafutwa

Serikali yaahidi kusimamia malipo ya wakulima

TCA yaahidi kununua pamba yote

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Marco Mtunga wa Pili kulia akishuhudia uzinduzi wa Msimu wa ununuzi wa pamba 2021/2022 uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Busega Bi Tano Mwera kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu

Msimu wa ununuzi wa pamba 2021/22 umezinduliwa rasmi tarehe 10 Mei 2021 huku serikali ikiahidi kusimamia haki ya mkulima, hasa kwenye matumizi ya mizani, na malipo ya wakulima kwa wakati. Uzinduzi wa msimu ulifanyika katika kijiji cha Mkula, kata ya Mkula wilaya ya Busega, huku wilaya hiyo ikitarajia ongezeko la asilimia 150 ya uzalishaji wa pamba mbegu kutoka tani 4,000 msimu uliopita hadi tani 10,000 msimu huu. Aidha katika msimu huu, serikali imefuta madeni yote ya pembejeo wasizokuwa wanadaiwa wakulima ambayo ni takriban shilingi bilioni 39.

Akitoa salamu za Bodi, Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Pamba, Marco Mtunga alisema, uzinduzi wa msimu umefanyika katika wilaya ya Busega kwa sababu uongozi wa Wilaya umeonesha juhudi kubwa katika kukuza na kuendeleza zao la pamba kwa kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto hususan utoaji wa elimu ya ugani kwa wakulima. “Halmashauri ilipeleka maafisa ugani na madiwani kwenye mafunzo katika Chuo cha Kilimo TARI Ukiriguru kujifunza mbinu bora za kilimo bora cha pamba ili waweze kutoa elimu hiyo kwa wakulima” alisemaMtunga na kuongeza kuwa tatizo la tija ndogo likipatiwa ufumbuzi kwa kutoa elimu ya upandaji bora wa pamba kwa wakulima, Busega ina uwezo wa kuzalisha takriban tani 50,000 za pamba mbegu.

Tatizo kubwa la kilimo cha pamba ni tija ndogo inasababishwa na maarifa duni waliyonayo wakulima wa pamba. Kutatua tatizo la elimu kwa wakulima, Bodi ya Pamba imewekeza katika kuwasaidia maafisa ugani katika maeneo yanayozalisha pamba ili waweze kuwafikia wakulima. “Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Zao la Pamba umeanza kutatizo tatizo la vyombo vya usafiri kwa maafisa Ugani. Maafisa ugani walio na pikipiki watapatiwa fedha ya mafuta na wasio navyo watapatiwa vyombo vya usafiri na mafuta. Aidha hadi kufikia tarehe 10/5/2021 takriban TZS milioni 85 zilmeshatumika kuwawezesha maafisa ugani na jumla ya pikipiki 22 zimetolewa” alisema Mtunga.

Akifafanua kuhusu umuhimu wa AMCOS kwa wakulima, Mtunga aliwaasa wakulima wanaojitenga na ushirika kwamba, kufanya hivyo ni kuendelea kulea ugonjwa ndani ya vyama vya ushirika. Ushirika imara unatokana na wananchi wenyewe. Matatizo makubwa ya AMCOS ni uongozi mbovu na ambao hautokani na wakulima. “Wakulima wakijiunga kwa wingi kwenye Ushirika watakuwa na uwezo wa kuchagua viongozi bora na hata kuondoa uongozi wasioridhishwa nao” alisema na kutoa mfano kuwa, katika msimu wa kilimo 2020/2021, kiwanda cha Chesano kilichoko wilaya ya Busega zilikamatwa takriban tani 20,000 ya mbegu zilizokuwa zimasambazwa kwenye AMCOS kwa ajili ya kupanda, lakini viongozi wasio waaminifu wakaziuza kwa ajili ya kwenda kukamua mafuta. Hali hii pia inatokana na ushirikiano mdogo kutoka kwa wananchi hasa pale wanapoona viongozi wa AMCOS wakifanya hujuma lakini hawatoi taarifa.

Aidha, katika hatua ya kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji, serikali imefuta madeni ya pembejeo ambayo walikuwa wanadaiwa. Katika msimu wa kilimo wa 2020/2021 Bodi ya Pamba kupitia Mfuko wa Kuendeleza Zao la Pamba ilisambaza mbegu za pamba, viuadudu na vinyunyizi kwa wakulima kwa njia ya mkopo.

Akitoa hotuba ya uzinduzi wa msimu wa ununuzi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Wilaya ya Busega Bi Tano Mwera, alisema uzalishaji wa pamba msimu huu wa 2021/2022 unatarajiwa kuongezeka mara dufu kutoka tani 122,836 msimu uliopita hadi kufikia tani 390,000. Ongezeko hili linatokana na juhudi kubwa zilizofanya na serikali kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba za kuhakikisha wakulima wanapata mbegu na viuadudu kwa wakati. “Msimu huu Bodi imesambaza viuadudu mchanganyiko kwa lengo la kukabiliana na ongezko kubwa la wadudu wanaofyonza pamba wanaotokana na mabadiliko ya tabia nchi” alisema Mwera na kuongeza kuwa , jumla ya chupa milioni sita (6) za viuadudu ziliagizwa na kusambazwa kwa wakulima na tani 12,000 ya mbegu za pamba zilizoondolewa mabaki ya nyuzi (delinted zilisambazwa kwa wakulima. Ni wakati sasa, wataalam kutafuta njia sahihi ya kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi hususan tatizo la wadudu kwenye pamba.

Mkuu wa Wilaya aliipongeza Bodi ya Pamba kwa kusimamia vyema zao la pamba hasa suala la uzingatia wa kanuni za upandaji wa pamba. “takriban asilimia 70 ya wakulima kwa sasa wanazingatia kanuni bora za kilimo cha pamba hususan upandaji wa pamba kwa mistari na kwa nafasi inayopendekezwa na wataalam” alisema Mwera na kuzishauri halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Bodi ya Pamba katika kuhakikisha tija katika kilimo cha pamba inaongezeka ili kipato cha mkulima na halmashauri kiweze kuongezeka.

Akiongea kuhusu kuwezesha maafisa ugani, mgeni rasmi aliipongeza Bodi ya Pamba kwa kuwapatia baadhi ya maafisa ugani vyombo vya usafiri na mafuta ya kuendeshea vyombo hivyo. Aidha aliombo uwezesho huu uwe endelevu ili wakulima wote wafikiwe kwa urahisi wakati wa msimu wa kilimo. “niziombe halmashauri za wilaya ambazo zinanufaika na ushuru unaotokana na zao la pamba, kutenga asiimia 20% ya ushuru kwa ajili ya kuwawezesha maafisa ugani kutekeleza majukumu yao. Alisema na kuongeza kuwa, wakati umefika kwa wanunuzi wa pamba wawekeze kwenye kilimo cha pamba na viwanda vya kuongeza thamani kwenye zao la pamba.

Kwa kuwa ununuzi wa pamba utafanyika kupitia AMCOS, niwaase viongozi wa AMCOS kuhakikisha wanazingatia sheria kanuni na taratibu za ununuzi wa pamba, kufuata kwa makini Mwongozo Na. 1 wa ununuzi wa Pamba msimu wa 2021/2022, kusimamia masilahi ya wakulima bila upendeleo, kusimamia usafi na ubora wa pamba na kutoa kipaumbele cha malipo kwa wakulima waliopimiwa pamba yao kwanza.