Habari

ZAO LA PAMBA NA UMUHIMU WAKE KIUCHUMI
Zao la pamba lina umuhimu wa kipekee katika uchumi wa nchikwani linatoa ajira kwa takriban asilimia 40 ya Watanzania wote katika mnyororo wa thamani. Mikoa 17 na wilaya 56 zinajihusisha na kilimo cha pamba. Takriban ekari 1,500,000 hupandwa pamba kila msimu. Zao la pamba linachangia pato la taifa la fedha za kigeni. Katika msimu wa 2019/2020 zao la pamba pamba ililiingizia taifa takriban dola za kimarekani milioni 243.07.
Pato linalotokana na pamba linaweza kuongezeka iwapo kutakuwa na utashi wa kisiasa wa kutaka kuwakwamua wakulima na kusimamia utekelezaji wa kanuni za kilimo.Iwapo sayansi itasimama mahali pake bila kuingiliwa na maslahi binafsi ya kisiasa, kitabadilika kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa cha kibiashara. Kama mkakati wa kutaka kuongeza tija na uzalishaji wa pamba, Bodi ya Pamba ilisambaza kamba maalum kwa wakulima wote wa pamba nchini ili kuwawezesha kupanda pamba kwa nafasi inayoshauriwa na wataalam. Hatua hii iliwezesha ongezeko la uzalishaji kutoka tani 122,362 za pamba mbeu msimu wa 2016/2017 hadi kufikia tani 348,977 za pamba mbegu katika msimu wa 2019/2020. Kutokana na kukosa msukumo wa kisiasa (political will), baadhi ya viongozi kushawishi wakulima kusia pamba na kuchanganya na mazao mengine, kukosekana pia kwa usimamizi madhubuti kutoka ngazi ya kijiji na uchache wa watumishi wa Bodi ya Pamba, baadhi ya wakulima wameachana na matumizi ya Kamba na kurudia tena kutumia njia za asilia za upandaji wa pamba hali ambayo inamfanya awe na mimea michache kwenye eneo na mwisho kupata tija ndogo sana.
Kwa vipindi tofauti tofauti Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na wadau wengine wa zao la pamba imebuni mifumo ya kumsaidia kupata pembejeo kwa njia rahisi, mifumo ambayo imesaidia kuongezeka kwa tija na uzalishaji wa pamba. Katika misimu ambayo uzalishaji umekuwa mkubwa, kumekuwa na mfumo mahususi wa kusimamia upatikanaji na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima. Katika msimu wa 2005/2006 hadi 2008/2009 kulikuwa na Mfumo wa “passbook” wa kumpatia mkulima pembejeo za pamba ambapo mkulima alijiwekea akiba ya fedha za kilimo wakati wa kuuza pamba na fedha zake kuhifadhiwa kwenye kitabu maalum. Kitabu hiki kilitumika kuchukulia pambejeo wakati wa msimu wa kilimo. Katika msimu wa kilimo wa 2012/2013 mfumo wa kilimo cha mkataba ulitumika ambapo vikundi vya wakulima viliingia kwenye makubaliano na mchambuaji wa pamba (Ginner); mkulima kumhakikishia mnunuzi upatikanaji wa pamba na mnunuzi kwa upande wake kumhakikishia mkulima upatikanaji wa pembejeo na huduma zingine; katika msimu wa 2019/2020, wakulima walipatiwa pembejeo zote (mbegu na viuadudu) kwa mkopo.
Upatikanaji wa pembejeo wa uhakika ni kigezo muhimu sana cha kuboresha uzalishaji wa pamba nchini hasa kwa kuzingatia kwamba wakati wa msimu wa kilimo wakulima wengi wanakuwa wamemaliza fedha za mauzo ya pamba za msimu uliotangulia hivyo kuwa vigumu kujinunulia pembejeo; na kwa kuwa kilimo chetu ni cha kujikimu ni mara chache sana kwa mkulima kuwa na akiba, na yule anayekuwa nayo kipaumbele cha kwanza ni mazao ya chakula hasa mahindi.
Waziri wa Kilimo Profesa Adolph Mkenda wakati akizungumza na watumishi wa Bodi ya Pamba hivi karibuni alisema, zao la pamba ni zao la kimkakati ambalo linalimwa kwenye ukanda wenye idadi kubwa ya watu hivyo kama taifa tunaweza kulitumia kama chachu ya kupunguza umaskini na kuchochea maendeleo iwapo changamoto ya upatikanaji na usambazaji wa pembejeo itapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Zao la pamba ni lazima tulivalie njuga kutokana na umuhimu wake kiuchumi” alisema Mkenda na kuongeza kuwa, tunahitaji kuuza pamba nje zaidi, tunahitaji kuwa na malighafi ya kutosha kwa ajili ya viwanda vya ndani hivyo tunahitaji kutumia uwezo mkubwa tulio nao kuongeza uzalishaji.
Katika mazungumzo yake na watumishi, Profesa Mkenda aliiagiza Bodi ya Pamba kuandaa andiko litakaloonesha jinsi mabadiliko yakiuzalishaji yamekuwa yakitokea, sababu zinazochangia kuongezeka na kushuka kwa uzalishaji na namna tunavyoweza kuondoka na hali hii. Pamoja na kuwa na mikakati mizuri kama taasisi, ni muhimu kwa malengo ya uzalishaji wa pamba yazingatie Ilani ya Chama Tawala kwa sababu ndiyo dira ya maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka mitano.
Uzalishaji wa mbegu usimamiwe vizuri ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora za kupanda. Kwa suala la pembejeo zingine hususan viuadudu serikali itaendelea kutafuta njia inayoweza kufanikisha uzalishaji wake hapa nchini ili kupunguza gharama kwa wakulima.
“Pamoja na ukubwa na sekta ya kilimo ; mchango wa kilimo kwenye pato la taifa ni asilimia 28 tu, ambapo theluthi mbili sawa na asilimia 70 ya Watanzania wotewanajihusisha na kilimo kama njia ya kujiendeleza kiuchumi. “ alisema Mkenda na kusisitiza kuwa, tija katika kilimo hususan pamba ni ndogo sana hali inayofanya mchango wa kilimo kuonekana mdogo sana licha ya kutoa ajira kwa watanzania wengi hasa wanaoishi vijijini.
“Kilimo ni suala la kimkakati kwa nchi yoyote duniani na lisiposimamiwa kwa umakini linaweza kusababisha athari kubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii” alisema Mkenda huku akifafanua kwamba katika baadhi ya mataifa duniani kilimo ni suala la usalama wa taifa ili kuhakikisha usalama wa chakula na maendeleo ya sekta zingine. Kila binadamu anategemea kilimo kwa namna moja ama nyingine, hivyo sekta ya kilimo kama sekta mtambuka isiposimamiwa na kuendelezwa ni vigumu sana kwa sekta zingine kuendelea.